Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Thursday, June 7, 2012

Kasulu yatoa ardhi kwa ranchi ya wanyama

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma imeingia mkataba wa miaka mitatu na kuipatia Kampuni ya Mawalla Trust Ltd ya mkoani Arusha, hekta 157,510 za ardhi kwa ajili ya mradi wa uwekezaji wa ranchi ya wanyama.

Utiaji saini huo ambao ulifanyika mbele ya wajumbe wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo katika uwekezaji huo utaiwezesha halmashauri kupata Sh milioni 440 kila mwaka kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii na kuhifadhi rasilimali za eneo hilo.

Akisoma mkataba huo mbele ya wajumbe wa kikao cha Baraza la Madiwani kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Kasulu, Mwanasheria wa Halmashauri, Alphonce Sebukoto alisema uwekezaji huo unalenga kuendeleza maliasili na uchumi wa wilaya hiyo.

Alisema kuwa miongoni mwa shughuli zitakazofanyika kwa mujibu wa mkataba huo ni pamoja na utalii wa uwindaji wanyama, kuangalia wanyama, upigaji picha, uendeshaji wa mahoteli na kambi za utalii.

Akizungumzia uwekezaji huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Adam Mawalla, wakili wa Kampuni ya Mawalla Trust Limited, Wilbright Mamkwe alisema kuwa uwekezaji unaofanyika unazingatia kuwafanya wanyama kuwa rafiki wa binadamu.

Alisema kampuni yake kabla ya kufanya uwekezaji huo imevifanyia vijiji vinavyozunguka ranchi hiyo mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuondoa migogoro na wananchi wanaoishi katika vijiji hivyo na kuwapa elimu kuhusu uwekezaji.

Alisema kuwa kampuni hiyo inayomilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania pamoja na mambo mengine, imelenga kuhakikisha wananchi wanaoishi karibu na eneo hilo la uwekezaji, wananufaika.

No comments: