Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, June 6, 2012

Bomu laua mtoto akilichezea Kigoma

MTOTO wa kijiji cha Kigadye, Kasulu mkoani hapa, Obedi Manase (8), amepoteza maisha baada ya kulipukiwa na bomu la kutupa kwa mkono alilokuwa akichezea na watoto wenzake wanne ambao wamejeruhiwa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Fraiser Kashai alisema jana mjini hapa kuwa ajali hiyo ilitokea mwanzoni mwa wiki kijijini hapo.
Alisema Obedi ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza wa shule ya msingi ya Kidadye na wenzake wanne ambao wamelazwa katika hospitali ya misheni ya kijiji cha Shunga ambao hali zao zinaendelea vizuri, walikuwa wakichezea bomu hilo bila kulitambua.

Alitaja waliojeruhiwa kuwa ni Tuju Seluke (7) aliyejeruhiwa tumboni, Sarah Manase (6) pajani, Enjo Seluke (4) sikioni na Isaka Yohana (4) jichoni.

Kamanda Kashai alisema uchunguzi uliofanywa na Jeshi hilo, ulibaini kuwa watoto hao waliokota bomu hilo lililokuwa limefichwa kwenye maua na baba mdogo wa marehemu aitwaye Ayubu James ambaye ametoroka na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Kijiji hicho ambacho kiko mpakani na Burundi, kimekuwa na mwingiliano mkubwa na watu kutoka nchi hiyo na kimekuwa kikumbwa na matukio mbalimbali ya milipuko.
Enzi za vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, kilikuwa moja ya vijiji ambavyo waasi wa nchi hiyo walikuwa wakikimbilia kujificha dhidi ya mashambulizi ya majeshi ya Serikali wakati huo.

Katika matukio mengine, Kamanda Kashai alisema jeshi lake kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji Mkoa, imekamata wahamiaji haramu 52 kutoka nchi za Maziwa Makuu ambao wamekuwa wakiishi kwenye vijiji mkoani hapa.

Alisema katika operesheni hiyo iliyofanyika kuanzia Mei 25 hadi Juni 5, wengi wa wahamiaji hao wanaotoka Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), walikuwa wakijishughulisha na uvuvi katika mwambao wa Ziwa Tanganyika.

No comments: