Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Friday, May 18, 2012

Watishia kuiburuza mahakamani Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Manispaa ya Kigoma Ujiji (KUWASA)

 Manispaa ya Kigoma Ujiji
Manispaa ya Kigoma Ujiji

WATUMIAJI wa huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Manispaa ya Kigoma Ujiji (KUWASA) wametoa siku 30 kwa mamlaka hiyo kurekebisha bei zinazotozwa vinginevyo wanakusudia kwenda mahakamani kupinga bei hizo.

Katika barua yao watumiaji hao wa huduma za Kuwasa wakiongozwa na wenyeviti wa mitaa 68 ya Manispaa ya Kigoma Ujiji wametaka uongozi wa mamlaka hiyo kusimamisha utozaji wa bei hiyo mpya iliyoanza Desemba mwaka jana na kuwa na nyongeza nyingine Machi mwaka huu hadi hapo watakapofunga dira za maji na mteja kulipia kiwango cha maji alicholipia ambacho kimesomwa kwenye dira hiyo.


Katibu wa Kamati hiyo, Bakari Songoro alisema kwamba kitendo cha mamlaka hiyo kutoza bei mpya bila kufanya marekebisho katika uboreshaji wa huduma zake ni ukiukwaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha pamoja kati ya mamlaka hiyo, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) na watumiaji hao wa maji katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.


Sambamba na kulalamikia bei ya maji pia watumiaji hao wamelalamikia kutokuwepo kwa mjumbe wa wananchi katika Bodi ya Kuwasa anayetokana na madiwani wa manispaa hiyo wakati wa mchakato wa kupandisha bei hiyo.


Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Kigoma Benedict Mosha alisema Mamlaka ya Maji inaonekana haina mkakati wa kutumia fedha zake katika uwekezaji wa uboreshaji wa huduma ya maji katika Manispaa Kigoma Ujiji na badala yake wanataka jambo hilo lifanywe na watumiaji maji.


Akijibu malalamiko hayo ya watumiaji maji, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa KUWASA, Mbise Jones alisema kuwa mamlaka yake imepokea barua hiyo ya kusudio kutoka kwa wateja wake na uongozi unaifanyia kazi na kwamba itatoa majibu kabla ya kumalizika kwa siku hizo.

No comments: