Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Thursday, May 17, 2012

Maharamia wasababisha kupanda bei ya samaki Kigoma

BEI ya samaki na dagaa wanaovuliwa katika Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma imepanda hali inayohusishwa na mapambano yaliyotokea hivi karibuni kati ya majeshi ya Tanzania na maharamia kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Katika mapambano hayo, boti ya maharamia hao ilizamishwa. Akizungumza na gazeti hili Mwenyekiti wa Wavuvi katika Mwalo wa Katonga, mjini Kigoma, Mada Mussa alisema kuwa upatikanaji wa samaki na dagaa umekuwa ni wa kiwango cha chini kutokana na vyombo vingi vya uvuvi kushindwa kufanya kazi.


Alisema kuwa moja ya sababu za kutofanya kazi kwa vyombo hivyo ni kushindwa kwa baadhi ya wamiliki kuwalipia vibali vya kufanya kazi na kuishi wafanyakazi wao kama ambavyo uongozi wa serikali mkoani Kigoma ulivyoagiza.


Mussa alisema kuwa sehemu kubwa ya watumishi wa vyombo vya uvuvi katika mwambao wa Ziwa Tanganyika mkoani kigoma wanatoka Burundi na DRC.


Alikiri kwamba wengi wa wafanyakazi hao walikuwa wakifanya shuguli hizo bila kukamilisha vibali vya kuwaruhusu kufanya kazi na kuishi nchini.


Mwenyekiti wa wavuvi katika Mwalo wa Kibirizi, Ramadhani Kanyongo alisema kuwa bei ya samaki imepanda kutoka Sh 12,000 kwa kilo hadi Sh 22,000.


Bei ya kasha moja la samaki imepanda kutoka wastani wa Sh 170,000 hadi Sh 370,000 huku bei ya samaki kwa bei ya rejareja ikipanda kutoka wastani wa Sh 3,000 hadi Sh 6,000.


Mwenyekiti huyo alisema sehemu kubwa ya vyombo vya uvuvi vimeshindwa kwenda kuvua sehemu ya mbali kwenye maji mengi ambako samaki wanapatikana kwa wingi na badala yake huvua maeneo ya karibu na wakati wa mchana.


Wakizungumzia hali hiyo baadhi ya wachuuzi wadogo wa samaki na dagaa katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, Asha Yusuph na Mwajuma Rashidi walisema kuwa tangu tukio hilo la uharamia, kumekuwa na changamoto kubwa kibiashara.

No comments: