Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, May 23, 2012

Wabunge wa Kigoma watembelea Uholanzi kujifunza uendeshaji wa sekta ya mafuta na gesi


Wabunge Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini), Yusuf Nassir (Korogwe Mjini), David Kafulila (Kigoma Kusini) na Sara Msafiri (Viti Maalum), wapo ziarani nchini Uholanzi kwa ajili ya kujifunza uendeshaji wa sekta ya mafuta na gesi.

Zitto jana aliandika kwenye mitando ya kijamii kwamba katika siku ya kwanza ya ziara hiyo, walielezwa namna leseni za biashara za mafuta na gesi zinavyotolewa na namna kodi zinavyokusanywa na kutumika.

“Tulielezwa kwamba serikali ya Uholanzi inapata jumla ya Euro bilioni 11 kama kodi kutoka kwenye sekta hii kwa mwaka hizi zikiwa ni takwimu za mwaka jana,” alisema.

Alisema serikali ya nchi hiyo ina hisa na inashiriki kwenye shughuli za kampuni hizo na kwamba haitumii mfumo wa uzalishaji shirikishi kama ilivyo kwa Tanzania ambako kampuni kwa kiasi kikubwa ni wakandarasi.

“Faida kubwa ya uzalishaji shirikishi ni kwamba dola inabakia kuwa mmiliki wa rasilimali; hata hivyo madhara ya mapato ya mfumo wa aidha, Kiholanzi au Tanzania, ni kiwango cha chini cha mapato kwa maana hiyo mifumo yote ni suala la kisemantiki tu,” alisema.

Zitto alisema suala muhimu kwa mifumo yote ni uongozi unaozingatia uwazi na uwajibikaji katika sekta nzima ya mafuta na gesi.

Katika ziara hiyo, Zitto alieleza kwamba wabunge hao wamekutana na Naibu Waziri Mkuu wa Uholanzi, Maxime Verhagen ambaye walimpa salamu kutoka Tanzania na kuahidi kwamba ushirikiano baina ya nchi hizo mbili ni endelevu.

“Nilimkumbusha kuhusu uhakika wa gesi asilia tuliyonayo inayofikia ujazo wa futi za ujazo trilion (TCF) 19 uliobainishwa kwenye ugunduzi wa visima vitano vinavyomilikiwa na kampuni ya BritishGas/Ophir pamoja na ile ya Songosongo, Mnazi Bay, Mkuranga na Nyuni wilayani Kilwa,” alisema.

Alisema alimweleza kiongozi huyo kwamba ni matumaini ya wabunge hao kuona kila Mtanzania ananufaika na utajiri wa nchi bila kuvuruga demokrasia na maendeleo yao.

Kwa mujibu wa Zitto, Naibu Waziri Mkuu huyo aliwahakikishia kwamba serikali yake ipo tayari kuisaidia Tanzania katika kuendeleza gesi iliyopo hususani ujuzi na kwamba baada ya majadiliano na ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje, ilikubaliwa kuanzisha ufadhili kwa Watanzania wanaoshughulika na sekta ya mafuta na gesi ili kuongeza wataalam.

Aliishauri Tanzania kutumia hazina hiyo ya gesi asilia kuendeleza miundombinu na kupunguza deni la taifa kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Jana Zitto na wabunge wenzake walitembelea maeneo mbalimbali ya gasi nchini humo kwa nia ya kujifunza mambo ambayo yanaweza kusaidia Tanzania katika kuandaa sera mpya ya gesi asilia na mipango ya sekta ya mafuta na gesi.

No comments: