Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, May 30, 2012

Manyovu Kigoma wataka mbolea ya kahawa

WAKULIMA wa Chama cha Ushirika cha Msingi cha Manyovu Amcos wilayani Kasulu mkoani Kigoma wameilalamikia Serikali kwa kushindwa kuwapatia mbolea ya ruzuku kwa zao la kahawa.
 
Wakizungumza katika mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika katika Kijiji cha Mkatanga, wamesema kwamba kwa miaka mingi wamejikuta wakitumia mbolea ya mazao ya chakula kwa zao la kahawa, kinyume na utaratibu uliowekwa na Serikali.
 
Suala la mbolea limewafanya wengi wao kushindwa kumudu gharama za kuhudumia mashamba yao ya kahawa kutokana na kuuzwa kwa bei ghali katika maduka ya watu binafsi, ikilinganishwa na ile ya ruzuku inayouzwa kwa bei nafuu.
 
Akijibu malalamiko hayo, Mwenyekiti wa chama hicho, Mathias Dangwa alisema  Serikali imeahidi kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo kwa lengo la kuwanufaisha wakulima wa kahawa ili wazalishe kwa wingi.
 
Hata hivyo, alisema kahawa haimo katika orodha ya mazao yanayopata mbolea ya ruzuku kwa vile malengo ya kutoa ruzuku kwenye mbolea ililenga kusaidia wakulima wanaolima mazao ya chakula.
 
“kutokana na malalamiko ya wakulima wa zao la kahawa tumelazimika kumuomba Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Magembe kutazama upya namna ya kuwasaidia wakulima wa mazao ya biashara kwa kuwa nao wanaliingizia taifa fedha nyingi za kigeni,” alisema Dangwa.
 
Pia katika kikao hicho kilichofanyika mwezi Aprili mwaka huu mkoani Morogoro, viongozi wa vyama vinavyolima kahawa waliiomba Serikali kuelimisha wakulima wa zao hilo kuzingatia vigezo vya ubora kwa lengo la kuipa hadhi kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.
 
Dangwa aliwaomba wakulima kuhakikisha wanakuwa makini na watu wasiozingatia vigezo vya ubora wa kahawa kwa kuwa kufanya hivyo kutaangusha sifa na thamani ya kahawa ya Kigoma ambayo kwa zaidi ya miaka miwili sasa imechaguliwa kama kahawa bora zaidi hapa nchini.
 
Ushirika wa Manyovu Amcos unaundwa na Wanachama kutoka Vijiji vya Mnanila, Mkatanga, Kibwigwa na Kitambuka ambao kwa sasa wameanza kuzalisha kahawa ya vikonyo inayouzwa kwa bei ya juu, yenye soko kubwa katika nchi za Ulaya Magharibi.

No comments: