Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, March 28, 2012

Wakimbizi wa Burundi mwisho Desemba 31 Kigoma


TUME ya pande tatu inayoundwa na serikali ya Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), imetangaza kufungwa kwa kambi ya Mtabila inayohifadhi wakimbizi wa Burundi ifikapo Desemba 31 mwaka huu.

Wakimbizi watakaobaki kambini hapo watashughulikiwa kama wahamiaji haramu.


Hayo yalisemwa na Waziri wa mambo ya ndani ya Tanzania, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa ushirikiano wa kitaifa, haki za binadamu na jinsia wa Burundi, Maitre Clotide Niragila katika mkutano wa pamoja na wakimbizi hao uliofanyika kwenye kambi hiyo iliyopo wilayani

Kasulu, Kigoma.

Nahodha alisema kuwa sababu tatu ambazo zinatambuliwa na sheria za kimataifa zinazowafanya wakimbizi hao kuendelea kupata haki za wakimbizi zimefikia mwisho na sasa

wakimbizi hao wanapaswa kurudi nchini mwao.

Alipoulizwa iwapo muda huo utapita na wakimbizi hao kuendelea kuwepo kambini hapo Waziri nahodha alisema kuwa wakimbizi hao watavuliwa hadhi ya ukimbizi na badala yake watachukuliwa hatua kama wahamiaji haramu kama ambavyo sheria zinafanyika kwa wahamiaji haramu wengine wanaoingia nchini.


Alisema kuwa zoezi la kuwarudisha kwa hiari nchini mwao wakimbizi hao litaanza Aprili Mosi mwaka huu na kufikia tamati Desemba 31.


Kwa upande wake Waziri wa ushirikiano wa kitaifa, haki za binadamu na jinsia wa Burundi, Maitre Clotide Niragila alitoa wito kwa wakimbizi hao kutosikiliza maneno ya upotoshaji na uongo yanayotolewa na watu wenye nia mbaya kwa maslahi binafsi katika jambo hilo.


Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Mwakilishi mkazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la

Kuhudumia Wakimbizi, Chansa Kapaya alisema kuwa jumla ya wakimbizi 37,000 wanatarajia kurudishwa kwao huku kila mwezi wakimbizi 5,000 wakirudishwa kupitia utaratibu wa tume ya pande tatu.

No comments: