Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, January 18, 2012

Mwandishi kizimbani Mjini Kigoma, adaiwa kufanya fujo


MWANDISHI wa habari wa kujitegemea mkoani Kigoma, Joctan Ngelly amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Mwandiga wilayani Kigoma akikabiliwa na mashitaka ya kufanya fujo na kuidharau Mahakama.

Baada ya kupandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka alikana na kupelekwa katika gereza la Bangwe mjini Kigoma kwa kuwa alikosa wadhamini licha ya dhamana yake kuwa wazi.


Mwandishi huyo alipandishwa kizimbani baada ya kukiuka onyo alilopewa awali na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Frederick Shayo wiki mbili zilizopita la kutoingia katika vyumba vya makarani na kutorudia kufanya fujo tena mahakamani hapo.


Mbele ya Hakimu Shayo, Karani wa Mahakama Ayubu Mababa alidai kwamba Joctan alifanya fujo na kuondoa utulivu ambao ungewezesha Mahakama kuendesha shughuli zake kwa utulivu.


Mwandishi huyo amefunguliwa kesi namba 8/2012 na alikumbwa na kadhia hiyo baada ya kumalizika kwa kesi yake ya msingi namba 163/2010 aliyowafungulia wananchi watatu wa Kijiji cha Mwandiga kwa kumtolea lugha isiyofaa.


Baada ya kukana mashitaka Hakimu Shayo aliiahirisha kesi hiyo hadi Januari 30 mwaka huu itakapoitwa tena mahakamani hapo.


Hiyo ni mara ya tatu kwa mwandishi huyo wa habari kupandishwa kizimbani tangu alipohamia mkoani Kigoma miaka mitatu iliyopita.


Pia anakabiliwa na kesi nyingine ya kumtukana Diwani wa Kata ya Kitongoni Manispaa ya Kigoma Ujiji, Kassim Zaidi iliyofunguliwa katika Mahakama ya Wilaya Kigoma.

No comments: