Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Sunday, December 18, 2011

Zitto- Mfumuko wa bei hatari kwa uchumi wa taifa

NAIBU Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Kabwe Zitto amesema mfumuko wa bei nchini ni tishio na unahatarisha uchumi wa Taifa na hivyo kutoa mapendekezo manne ili kuuhami uchumi na kupunguza upandaji wa kasi wa gharama za maisha.

Zitto, ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Fedha, aliyasema hayo katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana na kueleza kuwa mkakati mahususi unatakiwa ili kubadili hali hiyo.


Miongoni mwa mapendekezo aliyoyatoa ni kutaka kuongeza uzalishaji wa chakula kwa kuweka mbinu za kukuza uchumi wa vijijini ikiwa kama njia mojawapo endelevu ya kupunguza mfumuko wa bei nchini.


“Serikali sasa iache maneno matupu kuhusu sekta ya uchumi vijijini kwa kuelekeza nguvu nyingi huko, bali iruhusu na ivutie kwa kasi na kutoa vivutio kwa wazalishaji binafsi wa Sukari na mpunga katika mabonde makubwa,” alisema mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini (Chadema).


Pia alitaka Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika na maofisa wake watoke ofisini na kuhimiza uzalishaji mashambani, fedha zielekezwe kujenga miundombinu ya barabara vijijini.


Aidha, Zitto amependekeza Serikali kununua chakula cha kutosha hasa mchele na sukari kutoka nje na kukisambaza kwenye soko ili kupunguza upungufu wa bidhaa katika masoko.


Pendekezo lake jingine ni kujengwa kwa kiwanda cha kutengeneza gesi ya matumizi nyumbani kwa haraka ili kupunguza bei ya gesi, kuepuka kuagiza gesi kutoka nje na hivyo kuokoa fedha za kigeni na kutengeneza ajira.


“Kupanda kwa bei ya gesi asilia kunatokana na kwamba Tanzania inaagiza gesi hii yote kutoka nje ilhali malighafi ya kutengeneza gesi ipo hapa, Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini liingie ubia na kampuni binafsi ili kuwekeza katika kiwanda cha kuzalisha gesi hatimaye kushusha bei,” alisema Zitto.


Pendekezo lingine alilolitoa ni kutaka ushuru wote unaokusanywa kwenye mafuta ya taa upelekwe Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ili kufidia kupanda kwa bei ya mafuta ya taa.


“Mfumuko wa bei katika bidhaa ya mafuta ya taa unatokana na uamuzi wa kuwianisha bei ya mafuta ya taa na dizeli ili kuondoa tatizo la uchakachuaji wa mafuta, tatizo limeondoka lakini wananchi wanaumia sana, uamuzi sahihi wa kisera ni kupanua huduma za umeme vijijini kwa kuipa fedha zinazotokana na ushuru wa mafuta ya taa Wakala wa Umeme Vijijini,” alieleza.


Alisema usambazaji wa umeme vijijini utaongeza shughuli za kiuchumi vijijini, kukuza uchumi wa vijijini, kuongeza mapato ya wananchi kwa kuongeza thamani za mazao yao na hivyo kupunguza athari za mfumuko wa bei.


Pia alitaka sera ya matumizi ya serikali iangaliwe upya kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi yasiyo ya lazima, na kuelekeza fedha nyingi zaidi katika uwekezaji umma .


Alisema mfumuko wa bei unasukuma Watanzania wengi zaidi kwenye dimbwi la umasikini na pia unapunguza uwezo wa Serikali kutoa huduma za jamii kupitia bajeti na hata kutimiza mipango ya miradi ya maendeleo kama miundombinu ya barabara, umeme, bomba la gesi na madaraja.


Alisema mfumuko wa bei umezidi kuongezeka hali ambayo inaonesha kwamba Bajeti ya Serikali iliyopitishwa na Bunge, Juni, imepunguza uwezo wa kununua bidhaa na huduma kwa takribani asilimia sita.


“Hii ni sawa na shilingi bilioni 780 kuyeyuka katika Bajeti katika kipindi cha miezi minne tu ya utekelezaji wa wake, kutokana na kasi hii dhahiri kwamba, ifikapo mwisho wa mwaka wa Bajeti ya Serikali itakuwa imepoteza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kununua bidhaa na huduma kwa zaidi ya robo ya bajeti yake,” alisema.


Alisema hali ni mbaya zaidi kwa wananchi kwani mfumuko wa bei za vyakula umekua kwa kasi kutoka asilimia 14.8 Julai hadi asilimia 24.7 Novemba, hivyo kumuumiza mwananchi ambaye kipato chake kipo pale pale.


Alisema kwa upande wa mfumuko wa bei wa mafuta ya taa na gesi asilia unapaa kwa kasi kama moto ambapo bei ya mafuta ya taa yamepanda kwa asilimia 71 kati ya Novemba 2010 na Novemba 2011, huku bei ya gesi asilia ikiwa imepanda kwa asilimia 35.


Alisema “tusipokuwa makini na kupata majibu sahihi ya tatizo la mfumuko wa bei za vyakula, wananchi wengi na hasa watoto watapata utapiamlo na Taifa kuingia gharama kubwa katika kuwapatia huduma ya afya”.


Alisema kuna hatari ya dhahiri kwamba ifikapo Januari mwakani, tutakuwa tumerejea mfumuko wa bei wa kiwango cha mwaka 1992 (asilimia 21.9) zisipochukukuliwa hatua za haraka na hata kuzidi mfumuko wa bei kiwango cha juu kabisa ambacho kilifikiwa mwaka 1994 (asilimia 33).

No comments: