Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Sunday, December 18, 2011

Wanaume Kigoma wasindikiza wake zao kliniki

KUMEKUWA na ongezeko kubwa la wanaume wanaowasindikiza wenzao kuhudhuria kliniki ya baba, mama na mtoto katika Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Mwakilishi wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Mkoa wa Kigoma, Leonida Leonald alisema hayo wakati wa kukabidhi vitendea kazi kwa timu ya waelimishaji na uhamasishaji afya ya msingi katika jamii ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Akitoa takwimu kuhusu mafanikio hayo, Leonald alisema katika kipindi cha hadi kuishia Oktoba mwaka jana, ni wanaume 15 tu waliowasindikiza wenzao wao kliniki katika wanawake 120 waliohudhuria kliniki.

Alisema baada ya uelimishaji na uhamasishaji kufanyika, hali hiyo imeadilika na hadi kufikia Novemba mwaka huu, wanaume 91 waliwasindikiza wenzao kliniki ambapo wanawake 96 walihudhuria kliniki.

Mwakilishi huyo alisema mafanikio hayo yanatokana na timu hiyo ya uelimishaji na uhamasishaji afya ya msingi jamii inayofanywa chini ya usimamizi wa WAMA katika kata saba za Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa WAMA kutoka Makao Makuu, Gloria Minja alisema baiskeli 30, miavuli, makoti ya mvua na viatu vya mvua, vimekabidhiwa kwa watendaji wa timu hiyo.

Minja alisema vifaa hivyo vimetolewa kuwasaidia watendaji hao wanaofanya kazi kwa kujitolea kuifikia jamii wakati wote wa majira ya mwaka na kazi kubwa iliyowafanywa na watu hao, imesaidia katika mchakato wa kusaidia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milennia.

Akikabidhi vifaa hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, John Mongela alitoa mwito kwa wajumbe wa timu hiyo ya uelimishaji kutumia vitendea kazi hivyo kuhakikisha vinafanya kazi iliyokusudiwa na kuifikia jamii kwa urahisi.

No comments: