Jaji Katarina Revocut, ameuonya upande wa utetezi katika kesi ya wizi wa Sh. bilioni 2.2 za Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa), inayomkabili kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rajabu Maranda na binamu yake, Farijala kutoa taarifa mapema kama hawatafika mahakamani.
Rajabu Maranda
Jaji Revocate alitoa amri hiyo baada ya upande wa utetezi kudai mahakamani kuwa Wakili Majura Magafu alikuwa mkoani Tanga akihudhuria kesi nyingine. Alisema hajui ni lini Magafu alipata taarifa ya kwenda Tanga, hivyo wawe wanatoa taarifa mapema.
Aliongeza kuwa wanajua kabisa kuwa Mwenyekiti wa Jopo Jaji, Fatuma Masengi, amehamishwa mkoani Arusha na ametumia garama zake kutoka huko kwenda Dar es Salaam. “Naomba apewe taarifa. Kuna siku upande wa utetezi utalazimika kulipia gharama pia za hasara ya ucheleweshaji wa kesi kwa sababu zisizo za msingi,” alisema Revocat.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Desemba 30, mwaka huu, kwa ajili ya kupangiwa tarehe ya kuanza utetezi.Mapema jopo la mahakimu watatu wanaosikiliza kesi hiyo, ambao ni Projestus Kahyoza, Fatma Masengi na Revocate, walitoa uamuzi kuwa washtakiwa hao walikuwa na kesi ya kujibu Akisoma uamuzi huo, Hakimu Revocate alisema kulingana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, umethibitisha bila kuacha shaka kwamba, washtakiwa hao wana kesi ya kujibu.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kula njama, kughushi, wizi, kuwasilisha hati za uongo na kujipatia ingizo la fedha kwa njia ya udanganyifu kwenye akaunti Sh. bilioni 2.2 mali ya BoT wakijaribu kuonyesha kampuni yao ya Money Planners imepewa idhini ya kukusanya deni la Kampuni ya B. Grancel ya nchini Ujerumani .
Washtakiwa hao pia bado wanakabiliwa na kesi nyingine za aina hiyo katika mahakama hiyo, ambazo zitaendelea kusikilizwa.
No comments:
Post a Comment