Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Sunday, November 20, 2011

Wafanyakazi TRL kutolipwa kifutajasho

SERIKALI imesema haitalipa kifuta jasho kwa wafanyakazi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na badala yake imesema anayeona hawezi kufanya kazi bila kulipwa kifuta jasho hicho, aache kazi.

Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu alisema hayo mkoani Kigoma wakati akizungumza na wafanyakazi wa kampuni hiyo katika Kituo Kikuu cha Reli mjini Kigoma alipokuwa kwenye ziara ya siku moja ya kutembelea Idara na taasisi zilizokuwa chini ya wizara yake.


Nundu alisema kwa sasa Serikali haina mpango wa kulipa kifuta jasho kwa wafanyakazi hao na mpango uliopo ni kuhakikisha kampuni hiyo inaboreshwa na kulifanya lifanye kazi kwa tija.


Mbali na kuwaambia wafanyakazi hao, pia Waziri huyo aliwaambia baadhi ya wabunge aliofuatana nao kwamba walichukulie suala hilo kwa uzito mkubwa na kuiunga mkono Serikali katika mkakati wake wa kuifufua kampuni hiyo badala ya kila siku kusikia kelele za wafanyakazi kuhusu malipo ya kifuta jasho.


Alisema kwa ustaarabu na unyenyekevu wa hali ya juu, mfanyakazi anayeona hawezi kuendelea kuitumikia kampuni hiyo kwa sasa aandike barua ya kuacha kazi na Serikali itamlipa mafao yake huku ikiwa tayari kuendelea na wafanyakazi watakaokuwa na moyo wa kuifufua reli.


“Ndugu zangu naomba niwe mkweli na huo ndiyo msimamo wa Serikali kwamba kwa sasa hatuna mpango wa kulipa kifuta jasho kwa wafanyakazi wa TRL, badala yake tunawataka watusaidie kufanya kazi wakati tukiwa katika utekelezaji wa mkakati wa kufufua shirika,” alisema Waziri Nundu.


Pamoja na mpango huo wa kuifufua kampuni hiyo, alisema kwa sasa Serikali haitanunua mabehewa na injini mpya kutokana na mchakato wake mrefu na kitakachofanyika ni kufufua vilivyopo na kununua kutoka nje ya nchi katika ambazo zilikuwa zinatumia injini na mabehewa vinavyoendana na reli zetu.


Hata hivyo, kauli hiyo ya Waziri Nundu imelalamikiwa na wafanyakazi hao wa TRL mkoani Kigoma wakieleza kwamba huo ni usaliti wa Serikali kwa wafanyakazi hao na inawakatisha tamaa.


Michael Richard na Kifutumo Francis, walidai kauli hiyo ya Waziri inawakatisha tamaa wafanyakazi katika kufanya kazi kwa ari na moyo na badala yake wamemuomba waziri huyo kutafuta njia ambayo itawezesha kupatikana kwa kifuta jasho hicho na wafanyakazi kulipwa.

No comments: