Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Saturday, October 22, 2011

Zitto, Ndassa, Makalla wana changamoto kubwa Simba

KLABU ya Simba imefanya uteuzi wa wajumbe wa kamati mbalimbali ndani ya klabu hiyo.

Uteuzi huo uliotangazwa na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Rage, wabunge Richard Ndassa wa Sumve, Amos Makalla wa Mvomero na Kabwe Zitto wa Kigoma Kaskazini waliteuliwa katika Kamati za Mashindano na Fedha.


Ndassa na Makala ni wabunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakati Zitto ni mbunge kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema).


Rage ni Mbunge wa Tabora Mjini kwa tiketi ya CCM.


Kwanza nimpongeze Rage kwa kuwaona wabunge wenzie na kuwateua kwa nafasi hizo, naamini kuwepo kwake bungeni kama Mwenyekiti wa klabu hiyo kwa namna moja au nyingine kumemuwezesha kujua uwezo wa wenzie kwa nafasi hizo.


Niwapongeze wabunge hao kwa kuteuliwa kwa nafasi hizo kwani naamni mbali ya kuwa wanachama wa klabu hiyo pia wanastahili kwa nafasi hizo.


Licha ya kuwawakilisha wananchi wao bungeni lakini pia watapata nafasi ya kuwawakilisha mashabiki, wanachama na wapenzi wa Simba popote walipo kuiletea klabu hiyo mafanikio zaidi.


Ndassa na Makala kama wajumbe wa Kamati ya Mashindano, michango yao ni muhimu kuifanya klabu hiyo kongwe kurejea mafanikio iliyowahi kuyapata miaka ya nyuma.


Moja ya mafanikio ni kufika fainali ya Kombe la Caf mwaka 1993 na hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.


Ni wazi watapaswa kwa kushirikiana na uongozi na benchi la ufundi la timu hiyo kuisaidia timu

kwa mawazo yao kurejea mafanikio yake, ikiwezekana kupata zaidi ya hayo.

Michango na mikakati yao ni muhimu kwa timu hiyo katika mashindano yote.


Kabwe kupitia Kamati ya Fedha ya klabu hiyo anapaswa kuijengea mazingira yenye wanachama na mashabiki wengi kujinasua kiuchumi kwa kuepukana na utegemezi wa watu wachache.


Pia kwa nafasi yake anapaswa kuhakikisha klabu hiyo inasimamia vizuri mapato yake yatokanayo na vyanzo mbalimbali viwe vya milangoni, mauzo ya wachezaji nje ya nchi

nakadhalika dhima kuu ni kuitegemeza klabu.

Lakini wabunge hawa wana changamoto kubwa inawakabili ambapo wanapaswa kutofautisha

maslahi yao ya kisiasa na maslahi ya kuendeleza soka ndani ya klabu hiyo, kwani soka na siasa zina mifumo tofauti hivyo kuwa na namna tofauti hata ya uchangiaji wa mada na vitu kama hivyo.

Wasije wakajikuta wanatumia nafasi zao hizo kujijenga kisiasa zaidi kuliko maendeleo ya timu hiyo ambayo ndio hasa suala la msingi lililowafanya wateuliwe kwa nafasi hizo, kwani kwa kufanya hivyo hawatawatendea haki mashabiki, wapenzi na wanachama wa klabu hiyo.


Simba ni klabu ya michezo hasa soka, hivyo haitakiwi kuwa na sura za kisiasa kwa maana ya wabunge hao sasa kujijengea umaarufu binafsi kupitia nafasi zao ndani ya klabu hiyo, badala yake watumia umaarufu wa katika siasa kuisaidia klabu hiyo.


Ukosefu wa umakini katika kutofautisha maslahi yao ya kisiasa na maslahi ya soka unaweza ukawagawa watu ndani ya klabu hiyo kwani wapo wa itikadi tofauti na kinachowaunganisha ni soka tu na sio nje ya hapo.

No comments: