Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Thursday, October 20, 2011

Zitto na mradi wa demokrasia jimboni kwake

MWANZONI mwa mwezi huu Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), alizindua jukwaa la viongozi wa vijiji wa jimbo.

Jukwaa hilo linahusisha wenyeviti na watendaji wa vijiji. Akizungumza kwenye uzinduzi wa jukwaa hilo na baadaye katika mahojiano na mwandishi wa makala haya, Zitto anasema wazo la kuundwa kwa jukwaa hilo, lilitoka kwake la lengo ni kuona namna gani atapata nafasi ya kukutana na viongozi hao.


Anasema kuwa katika muundo na sheria za serikali za mitaa, hakuna chombo chochote ambacho kinawakutanisha viongozi hao wa vijiji na mbunge wao kwa pamoja ili kuweza kuzungumzia masuala ya maendeleo katika jimbo lao.


Mbunge huyo anabainisha kwamba wakati akitafakari jambo hilo, aliona kuwa Diwani anayo

nafasi ya kukutana na viongozi wenzake wa kuchaguliwa katika kikao cha kamati ya maendeleo ya kata na mbunge uwezo wake ni kuonana na madiwani katika kikao cha baraza la madiwani.

Kutokana na mlolongo huo, anasema kuwa hakuna mahala ambapo mbunge anaweza kukutana

na viongozi wa vijiji kwa maana ya watendaji na wenyeviti, zaidi ya mbunge kutembelea maeneo yao, jambo ambalo kama ana kitu cha kuongea kwa pamoja hakiwezi kupata nafasi.

Zitto anasema kuwa kabla ya kuanzishwa kwa jukwaa hilo, ulifanyika utafiti wa kuona namna

gani jambo hilo linawezekana ndipo alipokabidhiwa mtaalamu mzoefu wa mambo ya serikali za
mitaa nchini, Silvestre Masinde, ambaye ndiye aliyetoa mwongozo wa uundwaji wa jukwaani hilo.

Lengo la jukwaa la viongozi wa vijiji Zitto anasema amelazimika kuunda jukwaa la viongozi wa vijiji ili kuimarisha Demokrasia na utawala bora katika ngazi za chini.


“Mara mbili kila mwaka tutakuwa tunakutana kujadili changamoto za maendeleo katika vijiji vyetu na jimbo kwa jumla, tutakuwa tunapeana taarifa kuhusu miradi inayofanyika ndani ya jimbo na kutekelezwa na vijiji vyetu,” alisisitiza.


Anaongeza kuwa tutakuwa tunakaguana kuhusu matumizi bora ya fedha za maendeleo katika vijiji vyetu (peer review) na pia kuona vikao vya kisheria vya mikutano mikuu ya vijiji na halmashauri za vijiji inafanyika.


Ili kuhakikisha kwamba malengo hayo yanafanikiwa, asasi isiyo ya kiserikali ya Kigoma Development Initiative (KDI) itakuwa inakusanya taarifa, kuhusu maendeleo ya demokrasia na uwajibikaji wa vijiji kuhusu utekelezaji wa mkakati wa kuleta maendeleo vijijini.


Katika kupanua wigo, mbunge huyo wa jimbo la Kigoma Kaskazini anasema kuwa jukwaa litatumika kushauriana na wabunge na madiwani kuhusu vipaumbele vya kimaendeleo katika jimbo na kuvipeleka katika vikao vinavyogawa rasilimali (baraza la madiwani na bunge).


Anabainisha kwamba jukwaa linakusanya viongozi wa wananchi (wenyeviti wa vijiji) na

Watendaji (maofisa watendaji wa vijiji), bila mwelekeo wa kichama katika utekelezaji wa majukumu ya jukwaa.

Anasema kuwa jukwaa hilo, linajumuisha wajumbe 64 ambao ni kutoka vijiji vyote vilivyomo

ndani ya jimbo la Kigoma Kaskazini, bila kujali kwamba anatoka CCM au CHADEMA.

Changamoto za maendeleo Zitto anasema kuwa jimbo la Kigoma Kaskazini, bado lina changamoto nyingi za kimaendeleo, hasa katika suala la elimu, kwani jimbo hilo liko nyuma ukilinganisha na majimbo mengine.


Anatoa mfano kwamba wakati jimbo la shule 80 za msingi, lina shule 14 za sekondari ambapo kati ya hizo kuna shule moja tu yenye kidato cha tano na sita. Anasema kuwa wamejitahidi

kuwa na zahanati katika kila kijiji katika vijiji 64 vilivyopo.

Lakini, jimbo zima lina vituo viwili tu vya afya, ukiacha miradi ya ujenzi wa vituo vingine vinne katika kata za Mahembe, Mkigo, Mwandiga na Kagunga, ambavyo fedha zake zimepitishwa na bunge hivi karibuni.


Kuhusu tatizo la maji, anasema kuwa bado jimbo hilo halijaweza kufikia kiwango cha kuwafanya wananchi wasihangaike, ingawa anashukuru baadhi ya maeneo ipo miradi ambayo imeondoa kero kwa wananchi.


Anaeleza kuwa sehemu kubwa ya wakazi wa mwambao wa kaskazini mwa ziwa Tanganyika,

wanajishughulisha na uvuvi, lakini bado shughuli za uvuvi hazijaweza kuondoa hali ya umasikini, kwani vifaa vingi wanavyotumia bado vya kizamani.

Mkoa wa Kigoma umejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii, kama Hifadhi ya Taifa ya Gombe,

ambayo ni maarufu kwa kuhifadhi Sokwe Mtu. Hata hivyo, bado vivutio hivyo havijatumika vya kutosha kama vyanzo vya mapato na kuondoa umasikini.

Umasikini kwa wananchi Kilimo ndiyo uti wa mgongo wa wakazi wengi wa jimbo hilo, lakini

hali si nzuri katika kilimo cha mazao ya kilimo na yale ya biashara, hivyo kushindwa kuwaondoa wakazi wa jimbo hilo kwenye umasikini.

Anasema kuwa kahawa inaweza kuwa mkombozi wa wakulima wa nyanda za juu za jimbo hilo, kutokana na kahawa inayozalishwa huko kushika ubora wa juu katika Afrika Mashariki na

Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mkakati sasa ni kuona wakulima wanaongeza uzalishaji na upatikanaji wa masoko ya uhakika.

Jukwaa na viongozi wa vijiji Pamoja na majukumu mengine, Zitto anasema kuwa uundwaji wa
jukwaa la viongozi wa vijiji, unalenga kuharakisha mchakato wa maendeleo katika jimbo hilo.

Akizungumzia viongozi wa vijiji, anasema kuwa kwa mwaka wa fedha 2011/2012 Halmashauri ya wilaya ya Kigoma imepitisha bajeti ya Sh bilioni 4.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi katika vijiji vya jimbo la Kigoma Kaskazini.


Anasema kuwa miradi hiyo lazima itekelezwe kwa wananchi. Wenyeviti wa vijiji na watendaji wao wanapaswa kuwa wa kwanza katika kusimamia kuhakikisha utekelezaji wa miradi hiyo inafanikiwa.


“Kumekuwa na uchakachuaji mkubwa unaofanywa na wataalamu wa halmashauri katika utekelezaji wa miradi, wakati mwingine bajeti inatengwa lakini mradi haufanyiki, hapa viongozi wa vijiji wanalo jukumu kubwa la kufanya,” anasema Zitto.


Zitto anasema kuwa ni lazima viongozi wa vijiji wawe chachu ya kuona kwamba fedha zilizotengwa kwa utekelezaji wa miradi katika maeneo yao zinafika na miradi inatekelezwa kama ilivyokusudiwa.


Kuwepo kwa jukwaa la viongozi wa vijiji, kutatoa fursa kupeana taarifa, kuhusu hali ya

utekelezaji wa miradi na pale itakapoonekana kuna miradi imehujumiwa wajumbe watoe taarifa kwenye jukwaa ili kuingilia kati na kuweza kuzuia hujuma zozote zinazotaka kutokea.

Mbunge huyo anasema baada ya kuanzishwa kwa wilaya ya Uvinza hivi karibuni, wilaya hiyo mpya itakuwa na halmashauri yake muda mfupi ujao, hatua itakayofanya jimbo lake na halmashauri yote kuathirika kimapato.


Anasema kuwa sehemu kubwa ya mapato ya Halmashauri hiyo, inatoka jimbo la Kigoma Kusini, ambayo itakuwa wilaya ya Uvinza. Kwa maana hiyo kuna changamoto kubwa ya

kuhakikisha kwamba rasilimali kidogo inayopatikana, inatumika vizuri.

Mradi wa umeme Zitto pia anazungumzia Mradi wa Umeme Vijijini, ambapo anasema kuwa katika bajeti hii serikali imepitisha kiasi cha Sh bilioni 5.6 kwa ajili ya kugharamia mradi huo, ambao utaanza katika muda mfupi ujao na kutekelezwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA).


Mradi huu utapita katika vijiji saba vya jimbo hilo, ukitokea Mwandiga. Anatoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa REA na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ili kuondoa haraka migogoro ya fidia na mambo mengine yatakayojitokeza.


Zitto anasema kuwa anaamini jukwaa la viongozi wa vijiji, litatumika kuimarisha mawasiliano na ushirikiano miongoni mwa viongozi, bila kujali itikadi zao za vyama, itakuza demokrasia vijijini na kuongeza uwajibikaji katika utendaji kazi kwa viongozi.


Kwa kunzia, Zitto aliwakabidhi viongozi hao orodha ya miradi ambayo itatekelezwa katika vijiji mbalimbali vya jimbo hilo kwa mwaka huu wa fedha wa 2011/2012, ikionyesha aina ya mradi, kijiji utakapotekelezwa na kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo Zitto hafichi hisia zake, kwamba jukwaa hilo si mahali pa kuendesha propaganda za kisiasa, kwani mwisho wa siku kiongozi ambaye atahusika na ubadhirifu, ataambiwa ukweli na atashitakiwa kwa wananchi, ambao watatumia njia za kidemokrasia kumuondoa madarakani.


Ukiacha Zitto, nilibahatika kuongea na baadhi ya viongozi wa serikali za vijiji, ambao walisema kuwa kuundwa kwa jukwaa hilo, kutatoa fursa kwao kusimamia mchakato mzima wa maendeleo ya maeneo yao.


Mmoja wa viongozi hao, Bernad Kumotola ambaye ni Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamhoza, anasema kuwa bado bado viongozi wengi wa vijiji hawajui wajibu wao na mipaka ya majukumu yao na ndiyo wanapata shida katika utekelezaji wa majukumu yao.


Kutokana na hilo, viongozi wengi wa vijiji hawajiamini, hasa katika masuala ya kitaalamu yanayohusisha wataalamu wa halmashauri, ambao nao hutumia udhaifu huo kufanya wanavyotaka.


Issa Fungameza ambaye ni Mtendaji wa kijiji cha Nyarubanda anasema kuwa ipo haja ya viongozi wa vijiji, kupatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo ili kuwafanya wawajibike kikamilifu katika kusimamia na kuleta maendeleo ya maeneo yao.


Jukwaa hilo la viongozi wa vijiji ni la kwanza la aina yake kuundwa nchini. Ni wazi kuwa litakuwa mfano wa utekelezaji wa ujenzi wa demokrasia na litatoa changamoto kwa viongozi wa vijiji na halmashauri katika kusimamia utekelezaji wa masuala ya utawala bora.

No comments: