Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Friday, October 28, 2011

Machungu niliyoonja kwenda Kigoma

Ama kwa hakika waswahili husema ‘Tembea Uone’ ama ‘Kutembea kwingi ni kujifunza mengi’. 


Hivi ndivyo ninavyoweza kusema kutokana na tathmini yangu ya safari yangu ya hivi karibuni kwenda Kigoma, maarufu kama Mwisho wa Reli. Katu sikutarajia kama ndugu zetu wa Kigoma, ndivyo wanavyopata tabu ya kusafiri kwenda kwao.


Hata hivyo huu ni mtizamo wangu tu, yawezekana kwao wao sio shida ya usafiri ni raha, kwa sababu nilibaini kuwa huo ndio utamaduni wa safari ya kwenda kwao - tangu na kabla ya nchi

hii kupata Uhuru miaka 50 iliyopita.

Tena ni bahati kwao, kwani je, kama Wajerumani wasingejenga hiyo reli, si wangekua wanaisikia tu Dar kwa maneno?. Kwa kuwa kusafiri kwenda kwetu Moshi ni saa saba mpaka nane sikufahamu lolote, kama kuna watanzania wanasafiri kwa saa zaidi ya 40 mpaka 50, eti wanarudi nyumbani kusalimu ndugu zao au ni kibiashara katika Tanzania hii!.


Sikuchukua kalamu kuandika makala hii, kuwajulisha eti kuwa nilisafiri kwenda Kigoma. La hasha! Bali nimeiandika kutokana na machungu niliyoyapata njiani wakati wa kwenda na kurejea Dar es Salaam.


Je maisha haya mpaka lini, iwapo sasa ni miaka 50 tangu tupate Uhuru mwaka 1961? Kwa hali ilivyo, huenda miaka 50 mingine ikafika ndugu zetu hawa wanasafiri kwa staili hii. Na kama sio hivyo, basi serikali na shirika la reli nchini wana majibu sahihi, juu ya usafiri huu wenye adha na karaha za kila aina .


Mtu aliyezoea kusafiri kwenda mikoa ya Kilimanjaro, anayepanda mabasi ya starehe kama vile Dar Express au Fresh Coach, basi akisafiri kwenda Kigoma kwa kutumia Reli ya Kati, huenda akala kiapo cha kutokanyaga tena huko.


Kwa hakika nilifurahi kusafiri na kuona mikoa ambayo nilikuwa naisikia tu kama vile Tabora, Singida na Kigoma. Lakini, je ni yapi hasa yaliyonisibu? Yapo mengi sana. Jambo la kwanza ni

namna abiria wanavyojazana katika mabehewa, kiasi cha kuhatarisha usalama wao wenyewe pamoja na mizigo.

Kwa uchunguzi wangu, behewa moja lina uwezo wa kubeba abiria 80 pekee, waliokaa katika viti. Lakini, jambo la kushangaza ni kwamba behewa moja linapakia abiria zaidi ya 100, wengi wakiwa wamekaa chini na wengine wamekaa juu ya viti, milangoni na eneo lenye maliwato.


Na katika behewa nililokuwamo la Namba C, nilihesaba abiria 105. Na hii ndivyo ilivyokua katika mabehewa mengine zaidi ya 10, yaliyokuwa yakivutwa na kichwa kimoja cha treni,

achilia mbali yale ya mizigo.

Naweza kusema kwamba hii sio huduma bora bali ni mateso makubwa, kwa sababu abiria aliyekata tiketi yake anahitaji kusafiri kwa amani na starehe ;na sio kwa kuzongwa namna hii kwa safari ndefu kama ya kwenda Kigoma.


Mimi napinga huduma hizi za shirika la reli. Pamoja na kupata shida, pia hewa ndani ya behewa ni shida, kwani inakuwa nzito kutokana na kujaa kwa abiria kupita kiasi. Watoto hupata shida, kwani hulazwa chini kwa sababu mama zao wanafika pahali wanakuwa amechoka kupita kiasi.


Utakuta mama mwingine amesafiri na watoto zaidi ya wawili na wote anawapakata ama

wengine wanasimama na kukaa chini kwa sababu pengine hana uwezo wa kuwakatia tiketi.
Inapofika usiku wa manane wanapotaka kulala, hapo ndipo tatizo huonekana dhahiri, kwa sababu ni lazima walale na hulazimika kulala chini ya viti.

Kwa uchunguzi wangu, abiria wengi huanza kujazana ndani ya treni katika vituo visivyo rasmi, ama vile vilivyo rasmi kwa kukata tiketi ama mkwa kudandia. Na hupata upenyo wa kudandia,

kwa sababu hakuna udhibiti maalumu pamoja na kwamba kuna askari wanaosafiri na treni pamoja na wakaguzi wa tiketi, maarufu kama TT.

Pia, zipo sababu nyingine zinazochangia abiria kupanda bila utaratibu maalum. Sababu hii ni kwamba milango haifungwi na hata ikifungwa, mingi haina vioo katika madirisha yake, hivyo abiria kama vile wanaume na vijana wenye nguvu, hupitia katika milango hii kwa kudandia, hata kama terni ipo katika mwendo kasi au ikiwa inaondoka katika kituo ilichosimama kwa mmuda mfupi.


Lakini, pia iwapo treni itasimama katika vituo maalum au visivyo maalum, basi yeyote anaweza kupanda akijua kwamba atalipa nauli akiwa njiani au anaweza kushuka katika kituo

alichokusudia bila hata kulipa nauli, ikiwa wakaguzi watachelewa kupita kufanya ukaguzi wao.

Hili jambo nililishuhudia na niliona abiria kadhaa wakipanda na kushuka katika vituo

wanavyotakat bila kulipa nauli. Jambo lingine lililonikera katika safari hii ni usafi ndani ya treni.

Hili ni jambo adimu katika mabehewa, kwani abiria wenyewe hawazingatii usafi kwani kila anayekula kile alichokinunua, atakula humo ndani na kutupa masalia yake humo, hususan vyakula vyenye asili ya maganda kama vile miwa, ndizi au chupa za maji.


Hali hii inatokana na ukweli kwamba hakuna utaratibu maalum wa kwawekea abiria vifaa vya kuhifadhi taka. Usalama wa abiria ndilo suala lingine muhimu lililonipa shaka kubwa, kiasi kwamba mimi binafsi nilikuwa na wasiwasi iwapo ningefika salama.


Naaam ilipofika usiku sana tangu tutoke Dar na tukikaribia maeneo ya Kilosa, ghafla alijitokeza kijana wa kamanda Mwema akiwa amevalia gwanda, kama Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Fujo (FFU) akitembea behewa moja baada ya jingine.


Akaanza kunadi na kusema jamani abiria. Hapa ninamnukuu “Ninawatahadharisha muwe makini na simu zenu za mkononi, hususan ninyi kina mama ambao simu zenu mnazining’iniza

shingoni pamoja na mikoba yenu mnayopakata hata watoto wenu muwapakate, lakini msiwafunike gubigubi, mbakishe kichwa kionekane ili vibaka wasije kumkwapua wakifiri ni mkoba”, akasema kwamba katika maeneo ya Kilosa, vibaka hupanda juu ya mabehewa na kukwapua simu za mikononi , mikate na mikoba.

Hii ni rahisi kwa sababu madirisha ya treni, hufunguliwa kwa upande wa juu na iwapo kibaka atapanda juu na kupitisha mkono wake, basi anaweza kuiba kwa urahisi. Afande Yule akatoa kisa kimoja cha kibaka kunyakua mtoto akidhani ni mkoba kwani mama yake alikua

amempakata na kumfunika gubigubi.

Hata hivyo kwa mujibu wa askari kibaka Yule alimrejesha motto baada ya kubaini kwamba sio alichokusudia hivyo akamning’iniza na abiria wakamdaka na kumrejeshea mama yake. Baada ya kutoa tahadhari yake afande aliendelea na kazi yake katika behewa jingine.


Loh kumbe maneno yale yalikua kweli kwani punde tu nilisikia kelele mwezi, mwizi behewa zima limehamaki. Kumbe alikua kibaka ameshanyakua mkate uliokua umening’inizwa juu nah ii ni miongoni mwa tabia za wasafiri wa kigoma na tabora kwani hutundika mikate yao juu

utadhani ni bekari.

Hata hivyo kibaka Yule hakufanikiwa kwani kijana mmoja mwenye misuli alifanikiwa kushika

ile mikate na kuirejesha ndani ya behewa. Usalama sio kwa vibaka wanaopanda juu ya mabehwa tu, bali hata ndani ya mabehewa ndio hatari zaidi, kwani mama mmoja nae alilizwa
pochi yake ikiwa na simu ya mkononi na sh 38,000.

Baada ya mama yule kubaini ameibiwa, papo hapo alizirai ikabidi wasamaria wema wamchangie fedha ambapo zilipatikana shilingi elfu 68. Kwa uchunguzi wangu wezi wanaoiba ndani ya abiria ni wale wanaodandia treni njiani, ambao wengi ni vijana wadogo tena wasioeleweka kwani punde waweza kumuona na ghafla akatoweka.


Lakini, pia wapo wanaouza bidhaa mbalimbali mle ndani ya treni, ambao huzunguka kila behewa. Kimsingi, abiria wazoefu wanasema kwamba wao pia hushiriki sana kuwaibia abiria hususan abiria wanapoua wamelala fofofo usiku wa manane treni ikikata mbuga.


Nilisema awali kuwa huduma zitolewazo na shirika hili sio bora. Nilisema hivyo kwa sababu kwa nini abiria anayekata tiketi apate shuruba za kila aina, tena katika safari ndefu namna hii

ya zaidi ya saa 44? Hii sio haki hata kidogo - ya kutoa huduma za safari!.

Usalama ni mdogo kwa sababu kila mmoja anaweza kupanda treni bila kujua. Pia, abiria hulazimika kuacha madirisha wazi kutokana na kukosa hewa na ndipo vibaka hutumia nafasi

hiyo.

No comments: