Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, August 23, 2011

Mamia ya wakimbizi wa Burundi waingia mjini Kigoma


Zaidi ya raia 600 wa Burundi wamevuka mpaka na kuingia nchini kuomba hifadhi ya ukimbizi baada ya kutokea mapigano kati ya watu wanaodaiwa ni waasi na majeshi ya Serikali ya Burundi katika vijiji vinavyopakana na Wilaya ya Kibondo Mkoa wa Kigoma.
Imeelezwa kuwa raia hao wa Burundi waliingia katika vijiji vya Mkarazi katika Kata ya Mabamba na Nyagwijima na Kiduduye katika Kata ya Mugunzu, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Diwani wa Kata ya Mugunzu, William Simbagiye, alithibitisha raia hao wa Burundi kuingia nchini kwa lengo la kupewa hifadhi ya ukimbizi kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama nchini kwao.
Mkuu wa Wilaya ya Kibondo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya, Dahn Makanga, alisema kuwa hali hiyo imetokana na watu wanaodaiwa kuwa ni waasi wa Burundi wakiwa na silaha kuvamia wananchi nchini humo na kuwapiga kisha kuwapora mali zao.
Akiwahutubia wananchi katika uwanja wa Maendeleo  ya Vijana mjini Kibondo juzi, Makanga aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kuwa watulivu katika kipindi hiki na kushirikiana na serikali katika kupata taarifa zitakazosaidia kuimarisha amani.
Alisema  baada ya raia hao wa Burundi kuingia nchini Ijumaa iliyopita wakitaka kupatiwa hadhi ya ukimbizi, Serikali iliwasiliana na viongozi wa majimbo ya Ruyigi na Cankuzo nchini Burundi na kuamua kuwarejesha kwao.
Kwa mujibu wa Makanga, kundi la kwanza la Warundi zaidi ya 100 liliingia katika kijiji cha Mkarazi na makundi mengine yyaliingia katika vijiji vya Nyagwijima na Kiduduye, lakini walizuiliwa na kurudishwa kwao na vyombo vya dola vya Tanzania.
“Hawa sio wakimbizi wamekimbia mapigano tu na kwa kuwa nchi yao ina amani, tumewarudisha baada ya kuzungumza na wenzetu wa Burundi,” alisema Makanga na kuongeza:
“Raia hao wa Burundi walikimbia kufuatia kikundi cha watu wanaodaiwa kuwa ni waasi kuvamia vijiji vya mpakani na kuanza kupiga watu na kupora mali huku wakifyatua risasi hewani hali miliyofanya watu kukimia hovyo na wengine kukimbilia hapa nchini.”
Hata hivyo, alisema tayari ulinzi umeimarishwa katika eneo la mpaka wa Tanzania na Burundi na kuwataka wananchi kuondoa hofu na kuendelea na shughuli zao kama kawaida.
Baadhi ya wananchi wameitaka serikali kushirikiana na serikali ya Burundi kukomesha vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na baadhi ya raia wa nchi hiyo ambao hushirikiana na baadhi ya Watanzania kuendesha vitendo vya uporaji katika vijiji vya mipakani.
Mmoja wa wakazi wa Wilaya ya Kibondo, Ernest Kasikala, alisema kuna haja ya kuwa na mazungumzo ya pamoja kati ya kati ya viongozi wa Tanzania na Burundi ili kukomesha vitendo vya uhalifu.
Mkoa wa Kigoma umekuwa ukihifadhi wakimbizi toka Burundi kwa muda mrefu, lakini baada ya amani kurejea nchini humo humo maelfu ya wakimbizi wamerejea kwao.
Kambi tano za wakimbizi wa Burundi takribani 500,000 hivi sasa zimefungwa baada ya kurejeshwa kwao kufuatia makubaliano yaliyofikiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Serikali ya Tanzania na Burundi.

No comments: