Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, May 23, 2012

Wabunge wa Kigoma watembelea Uholanzi kujifunza uendeshaji wa sekta ya mafuta na gesi


Wabunge Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini), Yusuf Nassir (Korogwe Mjini), David Kafulila (Kigoma Kusini) na Sara Msafiri (Viti Maalum), wapo ziarani nchini Uholanzi kwa ajili ya kujifunza uendeshaji wa sekta ya mafuta na gesi.

Zitto jana aliandika kwenye mitando ya kijamii kwamba katika siku ya kwanza ya ziara hiyo, walielezwa namna leseni za biashara za mafuta na gesi zinavyotolewa na namna kodi zinavyokusanywa na kutumika.

“Tulielezwa kwamba serikali ya Uholanzi inapata jumla ya Euro bilioni 11 kama kodi kutoka kwenye sekta hii kwa mwaka hizi zikiwa ni takwimu za mwaka jana,” alisema.

Alisema serikali ya nchi hiyo ina hisa na inashiriki kwenye shughuli za kampuni hizo na kwamba haitumii mfumo wa uzalishaji shirikishi kama ilivyo kwa Tanzania ambako kampuni kwa kiasi kikubwa ni wakandarasi.

“Faida kubwa ya uzalishaji shirikishi ni kwamba dola inabakia kuwa mmiliki wa rasilimali; hata hivyo madhara ya mapato ya mfumo wa aidha, Kiholanzi au Tanzania, ni kiwango cha chini cha mapato kwa maana hiyo mifumo yote ni suala la kisemantiki tu,” alisema.

Zitto alisema suala muhimu kwa mifumo yote ni uongozi unaozingatia uwazi na uwajibikaji katika sekta nzima ya mafuta na gesi.

Katika ziara hiyo, Zitto alieleza kwamba wabunge hao wamekutana na Naibu Waziri Mkuu wa Uholanzi, Maxime Verhagen ambaye walimpa salamu kutoka Tanzania na kuahidi kwamba ushirikiano baina ya nchi hizo mbili ni endelevu.

“Nilimkumbusha kuhusu uhakika wa gesi asilia tuliyonayo inayofikia ujazo wa futi za ujazo trilion (TCF) 19 uliobainishwa kwenye ugunduzi wa visima vitano vinavyomilikiwa na kampuni ya BritishGas/Ophir pamoja na ile ya Songosongo, Mnazi Bay, Mkuranga na Nyuni wilayani Kilwa,” alisema.

Alisema alimweleza kiongozi huyo kwamba ni matumaini ya wabunge hao kuona kila Mtanzania ananufaika na utajiri wa nchi bila kuvuruga demokrasia na maendeleo yao.

Kwa mujibu wa Zitto, Naibu Waziri Mkuu huyo aliwahakikishia kwamba serikali yake ipo tayari kuisaidia Tanzania katika kuendeleza gesi iliyopo hususani ujuzi na kwamba baada ya majadiliano na ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje, ilikubaliwa kuanzisha ufadhili kwa Watanzania wanaoshughulika na sekta ya mafuta na gesi ili kuongeza wataalam.

Aliishauri Tanzania kutumia hazina hiyo ya gesi asilia kuendeleza miundombinu na kupunguza deni la taifa kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Jana Zitto na wabunge wenzake walitembelea maeneo mbalimbali ya gasi nchini humo kwa nia ya kujifunza mambo ambayo yanaweza kusaidia Tanzania katika kuandaa sera mpya ya gesi asilia na mipango ya sekta ya mafuta na gesi.

Monday, May 21, 2012

Walimu 347 Kigoma ruksa kujitoa CWT


TUME ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), imekubali ombi la walimu 347 wa Manispaa ya Kigoma Ujiji kujitoa kutoka katika Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ili kuanzisha chama kitakachotetea maslahi yao kutokana na madai kwamba chama hicho cha walimu hakikuwa na msaada kwao katika kutetea maslahi yao.

Akitoa uamuzi wa shauri hilo mjini Kigoma, mwamuzi wa shauri hilo, L.L Mwakyusa alisema baada ya mlolongo mzima wa uamuzi wa pande zinazohusika, Tume imeamua kuwa walalamikaji si wanachama wa CWT tena na kitabaki kuwa wakala kwa walalamikaji kwa kuwa ni chama pekee kinachotambuliwa na mwajiri.


Aidha, Mwakyusa alisema suala la makato kwa walimu hao linapaswa kuangaliwa upya kwa kuwa pande hizo zimeshaingia kwenye mgogoro na kwamba walimu hao hawatafaidi matunda halisi kama wanachama.


Pamoja na uamuzi wa kujitoa kwa walimu hao na kujiunga na chama kingine, alisema walimu hao wataendelea kukatwa ada ya uwakala ili kufaidi matunda ya masuala ya jumla kama walimu yatakayosimamiwa na CWT kwa mujibu wa kifungu cha 72 (c) cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya Mwaka 2004.


Akizungumzia hukumu hiyo, kiongozi wa kundi hilo la walimu, Kalimwabo Sabibi alisema pamoja na Tume hiyo kuridhia kujitoa CWT, wanakusudia kuanzisha chama kingine cha walimu kitakachosimamia maslahi yao.


Sabibi alisema kwa muda mrefu, walimu wamekuwa kama watoto yatima kutokana na CWT ambacho machoni kinaonekana kama kinasimamia maslahi yao, kudai hakifanyi chochote kwa ajili ya maslahi ya walimu.


Alisema walimu wamekuwa kwenye malumbano ya kudai maslahi yao kutoka kwa mwajiri badala ya chama hicho kuwa upande wao, wakati mwingine kimechangia kuwafanya wakose hata kile kidogo wanachodai.


Pamoja na hukumu hiyo, hata hivyo walimu hao wamesema hawajaridhishwa na uamuzi wa Tume kuruhusu kuendelea kukatwa kwa makato kutoka katika mishahara yao kwa ajili ya kuchangia CWT kwa kigezo cha ada ya uwakala wakati wao si wanachama wa chama hicho.

RC azuia uuzaji kahawa kwenye madebe Kigoma


 Mkuu wa Mkoa Kigoma, Issa Machibya

MKUU wa Mkoa Kigoma, Issa Machibya amepiga marufuku kwa wakulima mkoani humo kuuza kahawa kwenye madebe.

Aidha amewaagiza wakulima hao kutoanika kahawa yao chini kwani kwa kufanya hivyo wanaiondolea ubora kwenye soko la dunia. Machibya alitoa maagizo hayo kutokana na michango mbalimbali iliyotolewa na wadau wa kahawa mkoani humo inayoonesha kuwa kutosimamiwa kwa sheria za uzalishaji wa zao hilo kumechangia kushusha ubora wa zao hilo.


Mkuu huyo wa mkoa alizitaka halmashauri za mkoa huo kwa kutumia mabaraza yao ya madiwani kutunga sheria ndogo za kusimamia zao hilo.


Alisema kuwa taarifa zinaonesha kuwa kahawa inayozalishwa mkoani Kigoma imekuwa ikipendwa maeneo mbalimbali duniani na wanunuzi wamekuwa wakiikimbilia lakini uzalishaji usiozingatia viwango vya ubora unachangia kuwakimbiza wanunuzi hao.


“Kwa sasa serikali ya mkoa itajiingiza kikamilifu kuhakikisha inasimamia kwa karibu uzalishaji unaozingatia ubora wa juu wa zao la kahawa mkoani Kigoma na hatutakubali kuona mtu mmoja anaturudisha nyuma katika hilo kwa kile kitakachotokea,” alisema .


Awali Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Wakulima wa Kahawa mkoani Kigoma (KANYOVU), Jeremia Nkangaza alisema kulegalega kwa sheria za usimamizi na uendelezaji wa zao hilo, k


Nkangaza alisema kumekuwepo mkanganyiko katika namna ya kushughulikia mifumo ya masoko ya kahawa mkoani humo lakini akaonya kuwa hakuna mnunuzi yeyote ambaye yuko tayari kununua kahawa isiyo na ubora.


Meneja wa Bodi ya Kahawa (TCB) mkoani Kigoma, Kaberwa Rutachweka alisema kuwa masoko ya kahawa yapo wakati wote hata kama wakati mwingine bei inakuwa imeshuka kwenye soko la dunia lakini kahawa yenye ubora wa juu haiwezi kukosa wanunuzi.
umechangia kushusha ubora wa zao hilo kwa msimu huu hali iliyosababisha wakulima kupata bei ya chini katika soko la dunia.