Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, April 11, 2012

35 walivyonusurika kufa katika Ndege ya ATCL Kigoma

Ndege hiyo ilipata ajali umbali wa takribani meta 70 kutoka njia ya kurukia katika uwanja wa ndege wa Kigoma wakati ikijiandaa kuruka kwenda Dar es Salaam kupitia Tabora ikiwa na abiria hao wakiwemo wafanyakazi sita na rubani Emmanuel Mshana na rubani msaidizi, Mbwali Masesa.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Kihenya Kihenya, aliwaambia waandishi wa habari uwanjani hapo jana kwamba uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mwisho wa njia ambapo ndege ilipaswa kurukia kulikuwa na matope na hali hiyo inaweza kuchangia ndege hiyo kushindwa kuruka na kusesereka na kutoka nje ya njia.


Pamoja na ajali hiyo, Kamanda alisema hakuna mtu aliyepoteza maisha na abiria wote wako salama na walipata mshituko na baada ya ajali hiyo timu ya madaktari kutoka hospitali ya mkoa waliwafanyia vipimo abiria hao.


Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege wa Mkoa wa Kigoma, Elipid Tesha, alisema baada ya ndege hiyo kuanguka magari ya Zimamoto yaliwahi eneo la tukio na kuimwagia maji kutokana na moshi uliokuwa ukitoka lakini hata hivyo haikulipuka.


Akieleza namna alivyoona ikiondoka uwanjani hapo, alisema akiwa katika kituo cha kampuni ya Synohadro inayokarabati uwanja huo aliona ndege imesimama katikati ya uwanja na baadaye kuondoka kwa kasi.


Alisema baada ya kuondoka kwa mwendo huo wakati ikikaribia kumaliza uwanja, aliona inasuasua kuruka na akabashiri kuwa huenda ikawa na matatizo na baada ya muda akaiona ikibiringika kwenye matuta nje ya njia ya kurukia.


Kutokana na ajali hiyo alisema utaratibu unafanywa kuhakikisha abiria waliokuwa wasafiri wanaendelea na safari zao kwa kuwatafutia ndege nyingine.


Mmoja wa abiria hao, Askofu Mkuu wa Kanisa la Inland Church of Tanzania, Silas Kezakubi, alisema waliondoka Dar es Salaam saa moja asubuhi na kuwasili hapa salama lakini wakati wa kutua alishituka kuona ndege hiyo inafunga breki ghafla kitu ambacho katika maisha yake ya kupanda ndege hakuwahi kuona.


Alisema baada ya kutua na kushusha abiria walipanda abiria wa kwenda Tabora na Dar es Salaam ambapo ilianza kuondoka kama kawaida na kuingia njia ya kurukia.


Askofu huyo aliongeza kuwa ndege hiyo iliondoka lakini ilipofika katikati ya uwanja ilisimama ghafla na baadaye kunguruma sana kabla ya kuondoka tena kwa kasi ili iruke, lakini walishangaa badala ya kuruka ikabingirika. Mbunge wa Kasulu Mjini, Agripina Buyogera, alisema Mungu ndiye aliwasaidia hadi kuokoka.


Wakati huo huo, Neophitius Kyaruzi anaripoti kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Athuman Mfutakamba, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.


kuhusu ajali hiyo, alisema ndege hiyo ilipata ajali baada ya kuacha njia katika barabara ya kuruka na kutua ndege kiwanjani hapo na ilipata uharibifu kwenye bawa na injini moja.


Alisema abiria na wafanyakazi walipelekwa hotelini mjini Kigoma wakati shirika hilo likifanya mpango wa kuwasafirisha kwenda Tabora na Dar es Salaam.


Alisema uchunguzi wa kina kuhusu chanzo cha ajali hiyo unafanywa na wataalamu wa ajali za ndege.

 

No comments: