Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi),David Kafulila
MBUNGE wa Jimbo la Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, ambaye Desemba 8 mwaka huu alienguliwa katika nafasi ya ukatibu mwenezi, huenda akavuliwa uanachama. Habari zilizolifikia gazeti hili jana zimeeleza kuwa mbali na kuvuliwa wadhifa huo, mbunge huyo, sasa anakabiliwa na hatua nyingine ngumu zaidi kisiasa, baada ya uongozi wa chama hicho kutaka kumvua uanachama.
Kwa mujibu wa habari hizo, hatua hiyo imepangwa kufikiwa Jumamasi hii, wakati Halmashauri Kuu ya chama hicho itakapoketi kwa dharura jijini Dar es Salaam kujadili mambo mbalimbali ikiwamo, suala la Kafulila. Katibu mkuu wa NCCR Mageuzi Samwel Ruhuza alithibitisha jana maandalizi ya kikao hicho cha dharura lakini, akasema agenda zake hazijapangwa.
"Ni kweli Halmashauri kuu imeitishwa kwa dharura Jumamosi hii jijini Dar es Salaam na baadhi ya wajumbe wameanza kufika," alisema Ruhuza na kuongeza: “Mkutano utafanyika keshokutwa (Jumamosi) lakini bado hatujapanga eneo tutakapofanyia. Tukipanga tutawajulisha waandishi wa habari,” alisema Ruhuza.
Alipoulizwa iwapo moja ya ajenda za mkutano huo ni kumjadili Kafulila, katibu mkuu huyo alisema kwamba hawezi kulizungumzia suala hilo sasa hadi muda mwafaka utakapowadia. Chanzo cha habari ndani ya chama hicho kimeeleza kuwa kanuni za nidhamu na usuluhishi za NCCR ukurasa wa 49, jedwali la saba kipengele cha kwanza na cha pili, zinaonyesha kuwa Kafulila anaweza kutimuliwa uanachama na huo baada ya kuondolewa uongozi.
Kwa mujibu wa chanzo hicho "Mtu yoyote anayetoa siri za chama nje ya vikao kama ni mara ya kwanza atapewa karipio kali au kuvuliwa uongozi na endapo akirudia mara ya pili, anavuliwa uanachama." Vyanzo zaidi vilidokeza kwamba ni kosa kwa mwanachama kumtuhumu kiongozi au mwanachama mwenzake kupitia vyombo vya habari (nje ya vikao vya chama) na kwamba, kufanya hivyo ni sawa na kukihujumu chama.
“Kafulila alitakiwa kupingana na Mbatia (Mwenyekiti) ndani ya vikao vya chama na siyo katika vyombo vya habari na sio yeye tu, wale wote waliohusika kufanya jambo hilo nao watahusishwa”, kilisema chanzo hicho na kuongeza: “Suala hili karibu litafikia tamati na kumaliza mvutano ndani ya chama; Kafulila kavunja kanuni nyingi za chama sijui itakuwaje ngoja tusubiri uamuzi.”
Kauli ya Ruhuza Awali, akizungumza na gazeti hili Ruhuza alisema hawezi kuzungumza mambo ya ndani ya chama kwa kuwa kwa kufanya hivyo naye atakuwa amevunja kanuni na taratibu za chama. “Ninachoweza kuhoji ni kitendo cha Kafulila kuzungumza na vyombo vya habari juu ya barua niliyompa, kulikuwa na ulazima gani wa kuzungumza habari hizo?,” alihoji Ruhuza.
Alisema barua hiyo alimuandikia tangu Desemba 8 mwaka huu, lakini iweje taarifa za yeye (Kafulila) kuvuliwa uongozi zianze kuibuka baada ya kukabidhiwa barua hiyo. “Nashindwa kuelewa amezipeleka katika vyombo vya habari kwa mtizamo gani, mimi ningeweza kuwaita waandishi na kuwaeleza suala hilo lakini niliona halina maana yoyote,” alisema Ruhuza. Ruhuza alisema kutokana na madaraka aliyopewa kikatiba, anaweza kuteua wajumbe wa Sekretarieti au kuwaengua bila kushauriana na mtu yoyote.
“Nina mpango wa kuiboresha hii idara (Uenezi) ili kuipa makali, atakapoteuliwa mtu mwingine wa kuziba nafasi hiyo vyombo vya habari vitaelezwa,” alisema Ruhuza Alipoulizwa kuhusu hatma ya Kafulila, alisema suala hilo hawezi kulizungumza bali linaweza kujadiliwa katika vikao vya ndani vya chama. Mbatia Akizungumza na Mwananchi Mbatia alisema hawezi kuzungumza masuala ya utendaji wa chama katika vyombo vya habari na kutaka atafutwe Katibu Mkuu, ili alizungumzie suala hilo.
“Mambo ya chama siyazungumzi katika vyombo vya habari nayazungumza katika vikao vya chama na nikifanya hivyo, nitakuwa nimekwenda nje ya kanuni na taratibu za chama,” alisisitiza Mbatia. Kauli ya Kafulila Kwa upande wake Kafulila alisema anachofahamu ni kwamba, mkutano wa Nec utakutana Februari 3, mwaka 2012 na katika mkutano huo, Mbatia ndiye atatakiwa kutoa maelezo ya ajenda iliyoibuliwa katika mkutano wa Nec uliofanyika Novemba 5 mwaka huu kama ni mpinzani ama kibaraka wa CCM.
“Wajumbe wa Nec walionyesha kutokuwa na imani na Mbatia tangu mkutano wa Nec wa mwezi uliopita, na walimtaka awasilishe utetezi wake kwa Katibu Mkuu , utetezi ambao utajadiliwa katika kikao cha mwakani,” alisema Kafulila. Alipoulizwa kuhusu kuzungumza mambo ya ndani ya chama katika vyombo vya habari Kafulila alihoji, “Mambo gani hayo ninayozungumza na vyombo vya habari? Chama ni vikao kaka, wewe muulize Ruhuza kama Mbatia ameshawasilisha utetezi wake”.
Kutokana na hali hiyo huenda mkutano huo ukaibua sura mpya ndani ya chama hicho kutokana na kwamba kuna baadhi ya wajumbe walionyesha kutokuwa na imani na Mbatia tangu katika mkutano wa NEC ulimalizika hivi karibuni.
Katika hatua nyingine Ruhuza amesema hali ya siasa ndani ya chama hicho sasa ni shwari na kwamba kitaendelea kuwashughulikia wanachama wake wanaoonekana kuwa ni kikwazo kwa kutengeneza makundi yenye lengo la kukibomoa. Alisema kuenguliwa kwa Mbunge huyo ni adhabu tosha na kwamba chama hicho kitaendelea kufanya mabadiliko makubwa ya uongozi.
Alisema chama cha NCCR ni chama kikongwe hapa nchini na kwamba wanataka kukijenga ili kiwe imara ndio mana wameamua kufanya mabadiliko ya uongozi ndani ya chama na kwamba kwa kuanzia wameanza katika nafasi ya Katibu Uwenezi kwa kumuondoa katika nafasi hiyo. “Chama chetu hakiwezi kuyumbishwa na watu wachache na kwamba tumeamua kufanya mabadiliko ambayo sasa tunatengua baadhi ya vitengo ndani ya chama na kuweka uongozi mpya ambao utawezesha kuinua chama,” alisema Ruhuza.
Aidha Ruhuza alifafanua kwamba kutokana na kazi ya ukatibu Uwenezi ndani ya chama kuhitaji muda mwingi kutekeleza majukumu yake ya kazi wameamua kumuondoa Mbunge huyo katika nafasi yake iliaweze kupewa mtu ambae atafanya kazi hiyo kwa muda wote wa kazi.
“Kama unavyo fahamu Kafulila ni Mbunge na anamajukumu mengi katika jimbo lake sasa hatuwezi kuendelea na nafasi hiyo ambayo inahitaji mtu wa kufanya katika muda wote wakazi ndio mana tumeamua kumpumzisha,” alisema Hata hivyo Katibu Mkuu huyo alisema suala la Kafulila sasa limekwisha na haipaswi tena kulizungumzia kwa sababu tayari chama kimeshatekeleza majukumu yake kwa kufuata Katiba ya chama hicho.