Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, December 21, 2011

Ruhuza adai Tendwa amekurupuka

SAKATA la kuvuliwa uanachama kwa mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila limezidi kuibua mjadala baada ya Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi Samuel Ruhuza kumjibu Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa kwa kusema anatoa kauli za kukurupuka.

Kwa upande wake, Kafulila amesisitiza kuwa yeye bado ni mbunge, licha ya chama chake kutangaza kumvua uanachama, mwishoni mwa wiki iliyopita na kwamba anakamilisha taratibu za kwenda jimboni kwake kwa ajili ya ziara ya kikazi.Kauli hizo ni mwendelezo wa mjadala kuhusu hatma ya mbunge huyo, baada ya chama chake cha NCCR - Mageuzi, kumvua uanachama hatua ambayo kikatiba, ikiachwa kama ilivyo inamfanya apoteze ubunge.

"Ninachoweza kusema ni kwamba watu wajue, mimi bado ni mbunge wa Kigoma Kusini na mwishoni mwa wiki hii, naenda huko kwa ziara ya kikazi," alisema Kafulila jana alipokuwa akizungumza na gazeti hili.
 
Kafulila alisema licha ya uamuzi wa Halmashauri Kuu (NEC) ya NCCR-Mageuzi kumfukuza uanachama, kuna michakato mingi inayoendelea ndani ya chama hicho kuhusu suala hilo.

"Nisingependa kueleza ni michakato gani, lakini ieleweke tu kwamba utekelezaji wa hatua ya kunifukuza ni mchakato usioweza kunifanya nikome sasa kuwatumikia wananchi wake," alisema.

Aliendelea, “bado naendelea na kazi kama Mbunge wa Kigoma Kusini, naomba wananchi watambue hilo.”

Ruhuza amjibu Tendwa
Hata hivyo, Ruhuza akizungumzia ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini kutaka suluhu ya jambo hilo, alisema "Tendwa, ni mtu wa kupenda kukurupuka katika kauli zake."

“Kwanza, siamini iwapo haya maneno yametoka kwenye mdomo wa Tendwa, ila kama ni  kweli inatoka mdomoni mwake, basi yeye amekurupuka na mtu anayependa kutoa matamko sawa na mtu aliyetoka usingizini,” alisema Ruhuza.

Alisema ikiwa Tendwa anadai kwamba ofisi yake haikupata mwaliko wa kuhudhuria kikao cha kumng’oa Kafulila, wakati akielewa kilichofanya hivyo ni kikao cha NEC ya chama ambacho yeye, (Tendwa) siyo mjumbe basi matamshi yake yana kasoro.

“Anazungumza kuhusu wajumbe batili, yeye amewajuaje na amewaona wapi? Orodha ya wajumbe wa NEC ipo ofisini kwake, anaelewa kabisa idadi yao na kila kitu, sasa sijui haya maneno anayapata wapi?,” alihoji  Ruhuza.

Ruhuza alienda mbali zaidi na kumuita Tendwa kuwa ni mchochezi wa migogoro ndani ya vyama vya siasa akidai kuwa, licha ya kusikia viongozi wa chama hicho wakitukanwa kwa muda mrefu, hakuwahi kuchukua hatua yoyote.

“Halafu leo anasema tutumie busara, kuna wakati alisema tulipata usajili bila kukaguliwa ikabidi tumpeleke mahakamani, akatuomba msamaha. Huyu anakurupuka usingizini anatoa matamko,” alisema Ruhuza.

Ruhuza alimshauri Tendwa kabla ya kuzungumzia suala hilo, asome  Katiba ya NCCR – Mageuzi ili kubaini  hatua zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya makosa yaliyofanywa na Kafulila.

Mbunge CCM
Mbunge wa Viti Maalum CCM, Sara Msafiri, alisema suala la Kafulila linapaswa kupewa uzito na si kwa mtizamo wa kisiasa pekee.“Utaratibu wa watu 30 kutofautiana na wananchi wa jimbo zima siyo jambo la kufurahia, hili jambo linahitaji busara zaidi,” alisema Msafiri.

Msafiri alisema kitendo cha NCCR-Mageuzi kumteua Hashim Rungwe agombee urais halafu baada ya muda mfupi kumwona hafai hata kuwa mwanachama, kinaonyesha udhaifu mkubwa kwa chama hicho.

“Mtu mliyemsimamisha kugombea urais hata mwaka haujaisha, mnamwona hafai tena hata kuwa mwanachama. Hii ni aibu na wananchi wanatakiwa kuwa macho na vyama kama hivi,” alisema Msafiri.

Hata hivyo, Ruhuza alijibu hoja hiyo akisema, “Leo unaweza kuwa na mtoto mzuri sana ,lakini kesho akawa mbaya mno. Kwa hiyo hata sisi mtu akibadilika kinachotakiwa ni kumchukulia hatua.”

Mwishoni mwa wiki iliyopita, wajumbe 38 wa NEC ya NCCR-Mageuzi waliamua kumvua uanachama Kafulila kwa tuhuma za kuongea mambo ya chama nje ya utaratibu wa vikao vya chama.Kafulila mbali ya tuhuma hizo pia  alituhumiwa kutaka kufanya mapinduzi ya kumg’oa madarakani mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia.

Hata hivyo, uamuzi huo wa kumvua uanachama umepata upinzani mkali kutoka kwa wasomi na wanasiasa mbalimbali ambao wamenukuliwa wakisema kuwa NCCR- Mageuzi walikurupuka na inafifisha demokrasia ndani ya chama.

No comments: