Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, December 20, 2011

Uamuzi wa kumukomoa David Kafulila NCCR Mageuzi ni ufisadi - Tendwa

MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa amevitupia lawama vyama vya siasa kwa kufanya uamuzi wa kukomoana na kusababisha gharama zisizo za lazima kwa taifa na kutolea mfano gharama za Uchaguzi Mdogo ambazo zinasababishwa na kuvuana uanachama,
akizifananisha na ufisadi.

Kauli yake imetokana na hatua ya mwishoni mwa wiki ya chama cha NCCR-Mageuzi kumvua uanachama mbunge wake wa Kigoma Kusini, David Kafulila, hatua ambayo ina maana amepoteza kiti hicho cha ubunge na sasa taratibu za Uchaguzi Mdogo zitafuatwa kwa mujibu wa Katiba.


Tendwa amesema ingawa yeye siyo mhusika wa gharama za uchaguzi, lakini Uchaguzi Mdogo

una gharama kubwa ambazo alisema si chini ya Sh bilioni 19 na uchaguzi kama huo unakuwa ni gharama kwa kuwa haukupangwa kufanyika.

Msajili huyo aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana baada ya kutoa mada ya uongozi kwenye mafunzo ya viongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa kuhusu uongozi, uwajibikaji na utawala bora.


Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu kuvuliwa uanachama kwa Kafulila, Tendwa alisema Katiba ya sasa hairuhusu mtu anapovuliwa uanachama kujiunga na chama kingine kuendelea na ubunge wake, hivyo ni lazima ufanyike Uchaguzi Mdogo kujaza nafasi hiyo.


“Sasa hizi bilioni 19 nani atakuwa amesababisha? Maana nyie ni mahodari wa kuandika

mafisadi na hili je ni ufisadi au ni nini?

Maana tusiwe mahodari wa kuisema Serikali, bali pia vyama vya siasa vinapaswa kuisaidia Serikali badala ya kuisababishia hasara,” alisema Tendwa na kuongeza:“Chama kufanya hivyo ni kupoteza sifa, nafikiri kuna adhabu nyingi ambazo zingeweza kutumika tofauti na kumfukuza

uanachama, maana hii ni hasara.

Sisi hatuingilii uamuzi wa chama, ila huo ni ushauri maana hata walichokuwa wakijadili kwenye vikao hatukijui.”


Tendwa alivitaka vyama vya siasa kutumia busara katika kufanya uamuzi badala ya kufanya

uamuzi wa kukomoana katika vikao vyao na hivyo kusababisha hasara kubwa kwa taifa ambazo si za lazima.

Msajili huyo alisema Kafulila anaweza kuomba rufaa ndani ya chama, lakini nje ya chama, pia

anao uhuru wa kwenda mahakamani na atakaposhinda kesi atakuwa mbunge wa wananchi wake.

Akizungumzia suala hilo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi wa

Chama Cha Mapinduzi, Nape Nnauye alisema yeye si muumini wa kuwafukuza wanasiasa vijana kwenye vyama vya siasa, bali ni muumini wa kuvitumia vyama vya siasa kuwalea vijana.

“Sisi tunategemea vijana wanakosea ila tukijenga utamaduni wa kuwafukuza wanasiasa

vijana katika vyama vyetu nani atawalea na nani atawaelekeza vijana?

Mimi si muumini kabisa, mtu mzima utasema sasa huyu ameshindikana, lakini vijana hapana,”

alisema Nape na kuongeza: “Kijana akikosea leo afundishwe.

Sasa angalia suala la Kafulila, aliondoka Chadema na wakamuita sisimizi na majina mengine ya

ovyo, baadaye amekwenda NCCR nao wamemfukuza, sasa aende wapi?”

Mafunzo hayo ya siku mbili yanawashirikisha viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa kwa

lengo la kuwaelekeza kuhusu mahusiano yao na wanachama, kuona ni jinsi gani vyama vinawajibika katika ulinzi na usalama wa taifa pamoja na kuangalia maadili ndani ya vyama vya siasa.

Kwa upande wake, Kafulila akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, alisema hana tatizo na uamuzi uliotolewa na chama chake, bali anatulia.


Aidha, Kafulila amesema baada ya siku mbili kuanzia jana, ndipo atakapozungumzia kwa undani suala hilo kwa kuwa kwa sasa kuna taratibu zinazoendelea kufuatwa.


“Isingekuwa vizuri kuzungumza kwa sasa, najua wengi wangependa kunisikia zaidi,

lakini sisemi kwa leo (jana),” alisema Kafulila aliyevuliwa uanachama Jumamosi iliyopita na
Halmashauri Kuu.

No comments: