MKAZI wa kijiji cha Kigendeka wilaya ya Kibondo mkoani
Kigoma, Godfrey Lizunga ambaye alikamatwa akituhumiwa kuwa na nyara za serikali
isivyo halali amefariki dunia akiwa katika mikono ya polisi.
Kamanda wa Polisi
Mkoa Kigoma, Fraiser Kashai akizungumza na waandishi wa habari jana
alithibitisha kufariki dunia kwa mtu huyo mikononi mwa polisi na kueleza kuwa
alikuwa akishikiliwa kwa siku kadhaa kutokana na tuhuma zinazomkabili.
Hata hivyo pamoja na kukiri kwa mtuhumiwa huyo ambaye ni
mkulima kufia mikononi mwa polisi, Kamanda Kashai alisema mtuhumiwa alifariki
dunia akiwa chini ya ulinzi wa polisi katika hospitali ya mkoa Kigoma Maweni
akipatiwa matibabu baada ya kuugua ghafla.
Siku moja kabla ya Kamanda Kashai kutoa taarifa hizo, vyanzo
vya habari kutoka Hospitali ya mkoa wa Kigoma, Maweni, vilimweleza mwandishi
madai kwamba kuna mtu ambaye ni mahabusi aliyefikishwa hospitalini na polisi
akiwa amekufa.
Alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa taarifa hizo Kamanda Kashai
alisema ni daktari pekee ambaye anaweza kuthibitisha kwamba mhusika amekufa au
la na kwamba hili lilifanywa wakati mahabusu huyo alipofikishwa hospitalini hapo.
Alisema ni kweli mahabusu huyo alitolewa kwenye mahabusu ya
kituo kikuu cha polisi mjini Kigoma akiwa hajitambui na wakati akipatiwa
matibabu alifariki dunia na hili lilithibitishwa na daktari hospitalini hapo.
Pamoja na kuthibitisha kufa kwa mahabusu huyo, Kamanda huyo
wa jeshi la polisi hakusema sababu iliyosababisha kifo chake kwa kuwa uchunguzi
wa kifo hicho unasubiri kufika kwa ndugu wa marehemu.
Aidha Kamanda huyo hakuwa tayari kuthibitisha kwamba pengine
kipigo alichopata kutoka kwa askari wa jeshi hilo ndicho kilichomfanya kuugua
kwake ghafla na kupelekwa hospitali ambako mauti yalimfika.
Machi 28 mwaka huu, Kijiji cha Kigendeka wilaya ya Kibondo
mkoani Kigoma marehemu na watuhumiwa wengine watatu walikamatwa na jeshi la
polisi wakiwa na vipande 28 vya nyama ya nyati, kongoni na nyamele kinyume na
sheria.
Katika tukio jingine, raia wa Burundi, Ndayisaba Michael
ameuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali kichwani na watu wanaoaminika
kuwa wanatoka Burundi ambao walikuwa wakifanya kazi za vibarua.
Kamanda Kashai alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya
saa 4:00 asubuhi katika kijiji cha Mahembe, Kigoma Vijijini na kwamba polisi
mkoani humo inawashikilia Ernest Ntigwakundi, Minani Joseph na Ntilakwigwa
Evarist kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo.
No comments:
Post a Comment