WANACHAMA na wananchi mkoani Lindi wametakiwa kujitokeza kwa
wingi ili kutumia vyema fursa za huduma za madaktari bingwa zinazoratibiwa na
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) katika Hospitali ya Mkoa ya Sokoine.
Mwito huo umetolewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi ambaye
pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Abdallah Ulega wakati wa uzinduzi wa mpango
maalumu wa utoaji huduma za matibabu kwa madaktari bingwa kutoka Hospitali ya
Taifa Muhimbili.
Madaktari bingwa ni wa magonjwa ya akinamama, wataalamu wa
upasuaji na magonjwa ya moyo,figo na shinikizo la damu.
Ni fursa adhimu ambayo wengi wetu hapa mkoani Lindi,
hatukuwahi kukutana nayo na sababu kubwa inawezekana ni uwezo wa kugharimia
safari ya kwenda huko wanakopatikana madaktari bingwa sanjari na mlolongo mrefu
wa taratibu za kitabibu ili kuwafikia, lakini wenzetu, yaani Bodi ya
Wakurugenzi, Menejimenti ya Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya wameiona changamoto
hii na niseme wazi kuwa mpango huu utakuwa unaokoa maisha ya watu wengi ambao
hawakuwahi wala kuwa na ndoto za kukutana na madaktari bingwa katika maisha
yao," alisema Ulega.
Huduma hizo zimepangwa kufanyika kwa siku saba. Aidha Kaimu
Mkuu wa Mkoa huo aliwataka madaktari wa Sokoine kushirikiana na madaktari
bingwa kujifunza ili kujiongezea ujuzi wa kitabibu ili watakapoondoka huduma
hizi zisitetereke bali ziboreke zaidi. Pia aliwataka wananchi kujiunga na Mfuko
wa Afya ya Jamii (CHF) ili waweze kunufaika kwa kupata matibabu.
Maradhi hayabishi hodi wananchi hivyo kwa kuchangia CHF
uhakika wa matibabu ni mkubwa na pia utachochea maboresho ya huduma za matibabu
kwenye vituo vya afya, zahanati hadi hospitali mkoa wetu" alisema Ulega.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF) Emanuel Humba alisema mpango huo maalumu wa kupeleka huduma za madaktari
bingwa kwenye mikoa ya pembezoni , umezingatia mahitaji ya msingi na ya wakati
kwani ni dhahiri wapo wanachama wetu wengi waliopo vijijini, wana mahitaji
makubwa ya huduma za madaktari bingwa.
Alisema Mfuko umewagharimia madaktari hao pamoja na utoaji
wa dawa na vifaa tiba, ili kufanikisha mpango huo wenye thamani zaidi ya
milioni hamsini na mpango huu maalumu utekelezaji wake umeanzia mkoani Lindi na
utakuwa ukitekelezwa kila baada ya miezi mitatu na wanachama wa Mfuko watapata
matibabu kwa kutumia kadi zao sambamba na wananchi watapata huduma kwa kupitia
utaratibu wa kawaida ambao utakuwa na nafuu.
Aliitaja mikoa ambayo iko kwenye mpango huu maalumu kuwa ni
Kigoma, Rukwa, Katavi, Mara, Pwani na Tabora, hivyo wanachama na wananchi kwa
ujumla wajitokeze ili waweze kutumia fursa hii muhimu na adimu kupata huduma za
matibabu za madaktari bingwa.
No comments:
Post a Comment