Asha Baraka |
Mafanikio ya Asha Baraka yamemfanya mwanamke huyo kuwa
tegemeo la chimbuko la vijana katika fani nyingine pia ambapo pia amekuwa
akitumika kama Jaji wa Mashindano ya Miss Tanzania,
ambapo aliteuliwa kufanya kazi hiyo muhimu na Kamati ya Miss Tanzania mwaka 2002, mwaka huo
mlimbwende Angela Damas akitwaa taji.
Aliposhinda taji hilo,
Angela alifuatana na Asha Baraka hadi Uingereza katika mashindano ya Dunia
akiwa msimamizi wake. Katika kudhihirisha kwamba amenuia kuwakomboa Watanzania
kwa kuzalisha ajira zaidi, Asha amefungua Kituo cha Redio kikijulikana kama Lake Tanganyika Redio, iliyopo mkoani Kigoma ambayo
itaanza kurusha rasmi matangazo yake mwakani.
Kuanza kwa matangazo ya kituo hicho kunatokana na kuendelea
vizuri kwa taratibu zinazotakiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ili
kuiwezesha redio hiyo kuruhusiwa kuanza kurusha matangazo yake, lakini yeye
mwenyewe akisema tayari majengo na vifaa vimekamilika.
Anaposimulia historia ya maisha yake na mipango yake ya
baadaye, Asha Baraka hasiti kueleza ndoto na azma yake ya kuwa Mbunge wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
panapo uhai. Anasema ndoto zake hizo hazikuanza leo, bali zilianza mara tu
alipojiunga na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Tabora mwaka 1980, akiwa
Kidato cha Kwanza.
Wakati huo akisoma katika shule hiyo ya sekondari, Asha
anasema hakuwa na dalili ya kupenda muziki, wakati huo umaarufu wake mkubwa
ulitokana na michezo kama mpira wa kikapu,
mpira wa pete lakini umaarufu zaidi ukitokana na ugwiji wa kutimua mbio
(riadha) akimudu mbio ndefu.
Anasema kutokana na shule hiyo kutengana tu kwa ukuta na
Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora, kuna wakati ambapo walitumia mwanya huo
kutumiana barua baina ya wanafunzi wa kike na wa kiume ili kuomba ‘kutoka’
kwenda muziki, ingawa yeye binafsi hakupendelea tabia hiyo.
“Akili na mawazo yangu yote yali kuwa kwenye mbio, na hii
iliniwezesha kushiriki mashindano mbalimbali ikiwemo mbio zilizojulikana kama Arusha Olimpic ambapo nilikimbia mbio hizo ndefu tukichuana
na shule nyingine. “Nakumbuka katika mbio zile sikuibuka mshindi ingawa
nilifanya vizuri sana
na huo ndio ulikuwa mwanzo wa mimi kuonekana kwa viongozi wa Timu ya Shirika la
Bima la Taifa (NIC),” anasema.
Anasema akiwa kidato cha pili kutokana na uwezo wake wa
kukimbia kuwa mkubwa alichukuliwa na Shirika la Bima, akiwa mwajiriwa katika
Kitengo cha Michezo.
“Kipindi hicho kila shirika la umma kulikuwa na sekta ya
michezo, kama vile, Bandari, Kiwanda cha Viatu
cha Bora, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na kampuni nyinginezo. “Kama
nilivyosema nilichukuliwa kama mwanamichezo katika shirika hilo, nikawa mwajiriwa huku nikisoma.”
Anasema aliendelea kufanya vizuri kupitia riadha, lakini
alishindwa kufika mbali zaidi kwa vile michezo hiyo ilikuwa haijapewa
kipaumbele zaidi kwa kipindi hicho. Akisimulia kujiingiza kwake kwenye bendi za
muziki, Asha anasema kulitokana na kaka yake Baraka kumiliki bendi mbili ya Mk
Sound ambayo ilikuwa maalumu kupiga muziki wa hotelini, na MK Beats ambayo ilikuwa
maaalumu kwa kupiga muziki nje ya hoteli.
Mwaka 1991 anasema kaka yake alishindwa kuendesha bendi hizo
na vifaa kuwekwa ghalani, ndipo alipoamua kuvichukua yeye na kuanzisha bendi
mpya. “Nilianza na wanamuziki wa Bendi ya Mk Sound, pamoja na baadhi ya vifaa
maana vingine vingi vilishaanza kuharibika.”
Akiwataja baadhi ya wasanii aliokuwa nao kuwa ni King Dodoo,
Nyoshi al Sadat na wengine, ambapo hata hivyo mwaka 1992 bendi hiyo ilivunjika
kutokana na ugumu wa kuiendesha. Anasema mwaka 1994 alianzisha upya bendi ya
African Stars kipindi hicho akiwa na akina Mafumu Bilal, bendi iliyodumu hadi
mwaka 1995 kisha ikavunjika.
Baada ya hapo mwaka 1997 akairudisha bendi ya African Stars
‘ Twanga Pepeta’ sasa akiwa na manguli kama
Luiza Mbutu, Ramadhan Masanja a.k.a Banza Stone na wengineo ambao waliifanya
Twanga kuanza kutambulika vilivyo kwenye tasnia ya muziki wa bendi.
“Kuanzia hapo bendi ikaanza kukua na kupeleka changamoto kwa
wafanyabiashara wengine na wao kuanza kumiliki bendi baada ya kuona mimi
nafanya vizuri,” alisema.
Anasema mwaka 2002 alipata nafasi ya kwenda Uingereza
kusomea masomo ya namna nzuri ya kutoa huduma kwa wateja kazini kwake NIC,
lakini aliitumia nafasi hiyo kusoma masomo ya ziada yanayohusiana na promosheni
na utawala akilenga kujitanua zaidi katika kufanya shughuli za bendi.
Anasema alikuwa akiingia darasani kwa masomo ya huduma bora
kwa wateja kuanzia saa tatu asubuhi hadi sasa nane mchana na baadaye anakwenda
katika chuo cha pili kuendelea na masomo ya muziki hadi saa 11 jioni. Anasema
katika siku za mwisho wa juma alikuwa anakwenda viwandani kufanya kazi kwa
ajili ya kujipatia kipato, fedha ambazo ni sehemu ya alizozitumia kuimarishia
pia bendi yake.
Akisimulia changamoto iliyojitokeza wakati Twanga Pepeta
ikiwa inavuma katika tasnia ya muziki, Asha anasema ni ile ya kuondokewa na
Banza wakati huo akitegemewa sana
kwa utunzi na uimbaji. “Tulikaa muda mrefu bila ya ‘kuchanganya’ kwani tulikuwa
tukijiuliza ni nani anaweza kuziba nafasi yake, halikuwa swali rahisi kupata
jibu,” alisema.
Anasema kuondoka kwa Banza kulimfanya kukuna kichwa na
kufanikiwa kumpata Ali Choki, ambaye hata hivyo wakati huo hakuna aliyejua kuwa
anaweza kufanya vizuri hadi kuziba pengo la Banza. Asha anasema baada ya hapo
alianza kuzoea na kubaini kwamba anapoingia msanii kwenye bendi pia anaweza
kutoka, jambo ambalo limekuwa likitokea hadi hii leo.
Zaidi ya kumiliki bendi ya African Stars pia Asha anamiliki
Kampuni ya African Stars Entertainment Tanzania (ASET), ambayo inashughulikia
masuala ya burudani. Anasema kupitia Kampuni ya ASET, ameshafanya matamasha
mbalimbali, kama la kumchangia Muhidini
Gurumo, kutengeneza Albamu ya Ali Choki ya kwanza akiwa na Gurumo, kuandaa
matamasha ya Family Day, Kimwana Manywele na mengineyo.
Zaidi ya muziki Asha anasema anajihusisha na masuala ya
siasa; “niliingia kwenye siasa nikiwa bado mdogo sana,” anasema. Anasema aliingia kwenye siasa
akiwa bado yupo shule, ambapo alijiunga na Jumuiya ya Vijana wa CCM, ambao
walikuwa wafanya kazi Shirika la Bima, wakati huo akiwa amemaliza shule na
kuajiriwa na shirika hilo
kutokana na umahiri katika riadha.
Baada ya hapo alijiunga na Umoja wa Wanawake Tanzania,
wakati huo Mwenyekiti wake akiwa Zainabu Kawawa. Anasema alikitumikia chama
hicho huku akiendelea kupanda polepole, hadi alipogombea nafasi ya Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Kinondoni kupitia UWT mwaka 1995, lakini akakosa
jambo ambalo halikumkatisha tamaa.
Hata hivyo alipata nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya
Wilaya, ambayo alidumu nayo mpaka mwaka 2005, mwaka ambao alifanikiwa kushinda
nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC).
“Hivi sasa matarajio yangu ni kuwa Mbunge, kupitia sehemu
yoyote ile ambayo nahisi naweza kuwania hata mkoani kwangu nilipotokea,”
alisema. Kama alivyofanikiwa kuingia NEC kupitia Wilaya ya Uvinza, Asha anasema
ndivyo anavyoweza kufanikiwa kuingia kwenye Ubunge kupitia jimbo hilo hilo.
“Siasa yangu ni siasa ya maendeleo ya vijana, wanawake, watoto na wazee ili
kukuza uchumi wao binafsi na uchumi wa nchi,” anasema.
Anasema muziki umemsaidia kujulikana sana na kufanikisha mambo yake madogo madogo
katika biashara zake, hasa baada ya kuacha kazi Bima Mei mwaka 2011. Hivi sasa
anakamilisha ujenzi wa Studio ya Muziki na Video, kwa ajili ya kutoa ajira zaidi
kwa vijana. Asha anasema bendi yake ina tuzo nyingi, karibu kila mwaka wanapewa
tuzo, lakini yeye mwenyewe amepewa tuzo mbili.
Tuzo ya kwanza walipewa na Msondo Ngoma mwaka 1995, ikiwa ni
tuzo ya kuendesha vizuri bendi na ya pili alipewa mwaka 2000 kupitia Wizara ya
Habari na Utamaduni ikiwa ni Tuzo ya Mwanamama Jasiri anayeendesha vizuri
bendi.
Huyo ndiye Asha Baraka, mtoto wa sita kati ya watoto 10,
aliyesoma Shule ya Msingi Nguruka Kigoma kabla ya kujiunga na Shule ya
Sekondari ya Wasichana ya Tabora maarufu kama
Tabora Girls.
No comments:
Post a Comment