UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Kigoma
umeunga mkono kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa hivi karibuni ya kutaka
viongozi wapimwe kutokana na utendaji wao wa kazi na wamemuomba kuwawajibisha
walioshindwa kutekeleza wajibu wao.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana Katibu
wa UWT Mkoa wa Kigoma, Mwajemi Balagama alisema kuwa viongozi wasiowajibika
wamepoteza sifa hivyo ni vema wakaachia nafasi zao ili zichukuliwe na wengine
wanaoweza kuwajibika ipasavyo na kuchochea maendeleo.
“Hivi sasa tunatakiwa kufanya kazi kwa ari zaidi, nguvu
zaidi na kazi zaidi. Wakati wa kufanya uzembe umepita, hivi sasa wananchi wetu
wanahitaji kuona maendeleo yanapatikana na kero zinatatuliwa na si kubweteka na
kutoa mwanya kwa wapinzani kutukosoa,” alisema.
Alisema UWT imejipanga kuhakikisha CCM inaendelea kushika
dola katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2015, kutokana na ukweli kwamba
idadi kubwa ya wapiga kura ni wanawake ambao wakiweka msimamo hawayumbi huku
akisema jitihada za kuongeza wanachama zaidi zinaendelea.
Umoja huo pia umetoa pongezi kwa Rais Kikwete kwa kutekeleza
ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni za mwaka 2005 kuhusu kuboresha umeme na
barabara ambapo hivi sasa matatizo hayo yametatuliwa na wananchi wameweza
kujiajiri kwa kufungua miradi midogo inayotumia nishati ya umeme.
No comments:
Post a Comment