IMEELEZWA kuwa umasikini unaowazunguka wananchi wanaoishi
kuzunguka ziwa Tanganyika mkoani Kigoma ndio chanzo cha kuharibiwa kwa ziwa
hilo, ikiwemo matumizi ya nyavu zenye matundu madogo maarufu kama kokoro.
Mkuu wa Wilaya Kigoma Ramadhani Maneno alisema hayo wakati
akikabidhi vifaa mbalimbali pamoja na pikipiki vyenye thamani ya shilingi
milioni 40 vilivyotolewa na mradi wa maendeleo ya bonde la ziwa Tanganyika kwa
taasisi ya utafiti wa samaki (TAFIRI) na idara za uvuvi katika Halmashauri ya
wilaya Kigoma na Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu.
Ili kukabiliana na hali hiyo, mkuu
huyo wa wilaya amesema kuwa juhudi za makusudi za kuwatafutia miradi ya
kiuchumi wananchi wanaoishi vijiji vya mwambao wa ziwa Tanganyika hazina budi
kuimarishwa.
Alisema kuwa kutokana na kuzungukwa
na umasikini baadhi ya watu wanaoishi katika vijiji vya mwambao wa ziwa
Tanganyika wamekuwa wakifanya shughuli za kuwaingizia kipato kwa haraka hata
kama shughuli hizo hakikubaliki kisheria na matokeo yake ni kuharibika kwa
mazingira ya ziwa.
Hata hivyo, alisema kuwa pamoja na
kutoa elimu na kuwapatia miradi mbalimbali ya kuwainua kiuchumi serikali
haitasita kuchukua hatua madhubuti kwa wote watakaokamatwa wakijihusisha na
shughuli ambazo zinasababisha uharibifu ndani ya ziwa Tanganyika.
Akizungumzia kutolewa kwa vifaa
hivyo, Kaimu Mratibu wa Taifa wa mradi wa maendeleo ya bonde la ziwa
Tanganyika, Magessa Bulai amesema kuwa vimelenga kusaidia kuwajengea uwezo
watendaji katika taasisi hizo kuweza kufika maeneo mbalimbali ya ziwa hilo kwa
ajili ya kusimamia shughuli za ulinzi na uhifadhi wa ziwa Tanganyika katika
shughuli za uvuvi.
Alivitaja vifaa vilivyotolewa kuwa ni
pamoja na pikipiki nne, seti ya vinakilishi ikiwa na printa yake kwa kila
taasisi, mashine kubwa ya kutolea nakala ambapo alisema kuwa pamoja n a
kusaidia usafiri pia vifaa hivyo vitasaidia uhifadhi wa kumbukumbu mbalimbali
za utendaji wa idara hizo.
Kwa upande wake afisa uvuvi wa
halmashauri ya wilaya Kigoma, Josephat Gowele amesema kuwa uvuvi haramu wa
kutumia makokoro bado ni changamoto kubwa kwa halmashauri yake na kwamba
kutolewa kwa vifaa hivyo kutasaidia kuimarisha doria za kila wakati na kupunguza
vitendo vya uvuvi haramu.
No comments:
Post a Comment