Kabwe Zitto (Chadema)
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), amemtaka
Spika wa Bunge, Anne Makinda, ang’olewe madarakani, baada ya kutangaza uamuzi
wa kuvunja Kamati ya Bunge aliyokuwa anaiongoza ya Hesabu za Mashirika ya Umma
(POAC).
Zitto aliyetuma taarifa kwa vyombo vya habari jana, alidai
Makinda amefanya uamuzi kwa kukurupuka, bila kuzingatia maslahi ya nchi wala
historia ya uwajibikaji katika nchi. “Ni lazima Spika wa Bunge adhibitiwe kwa
kuondolewa katika nafasi hiyo haraka iwezekanavyo. Spika lazima ajue kwamba
Mamlaka yapo kwa wananchi na yeye ni msimamizi tu wa vikao vya Baraza la
wananchi liitwalo Bunge,” alidai Zitto.
Alisema kuvunjwa kwa POAC, kunarudisha nyuma maendeleo
makubwa ya kujenga Bunge imara na lenye meno. Badala yake, alitaka POAC
iongezewe nguvu zaidi, ili idhibiti uwezekaji wa Serikali kwenye kampuni
binafsi badala ya kuifuta. Alitoa mfano wa uwezekaji wa Serikali kwenye kampuni
kama BP, AirTel, Kilombero Sugar na Songas, aliodai hauna uangalizi wowote.
Zitto katika taarifa hiyo, amejinasibu kuwa katika miaka
mitano iliyopita, POAC imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa umahiri na kwa
uwazi kuliko kamati nyingine zote za Bunge. Katibu wa Bunge Akizungumzia uamuzi
huo wa Spika, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah alisema haukufanywa na
Spika peke yake, bali ni baada ya kushauriana na Kamati ya Kanuni za Bunge
ambayo iliridhika na sababu za kufanya hivyo.
Wajumbe wa kamati iliyoridhia makubaliano hayo mbali na
Spika na Naibu Spika, Job Ndugai, wengine ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani
Bungeni, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema). Wengine ni Mbunge
wa Mbulu, Mustapha Akunaay (Chadema), Mbunge wa Kibondo, Felix Mkosamali
(NCCR-Mageuzi), Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF) na Mbunge wa
Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF).
Pia, yupo Mbunge wa Viti Maalum, Anna Abdallah (CCM), Mbunge
wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo
Makani (CCM), Mbunge wa Viti Maalum, Pindi Chana (CCM) na Mbunge wa Musoma
Vijijini, Nimrod Mkono (CCM). Dk Kashilillah alisema mabadiliko hayo
hayakuigusa kamati ya POAC peke yake, bali pia yalizigusa kamati zingine kama
ya Sheria Ndogo na ile ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje, ambayo imevunjwa na
kugawanywa mara mbili.
Sababu Akielezea sababu za kuvunja POAC, Dk Kashilillah
alisema lengo ilikuwa ni kuunganisha wizara, taasisi zake pamoja na mashirika
yaliyo chini ya wizara husika, ili yawe na msemaji mmoja. Alisema awali Waziri
na taasisi zingine za Serikali walikuwa wanawajibika kwa Kamati ya Hesabu za
Serikali (PAC), wakati mashirika ya umma yaliyo chini ya Wizara yakiwajibika
chini ya POAC.
Kwa mujibu wa Dk Kashilillah, kulikuwa na mkanganyiko mkubwa
na akaeleza kuwa hatua ya kuunganisha wizara na mashirika yake ya umma,
kutafanya sasa Waziri, Katibu Mkuu, Mwenyekiti wa Bodi pamoja na watendaji
wakuu wa mashirika, kuwajibika kwa kamati moja ya PAC. Dk Kashilillah alisema
sababu nyingine ni kuangalia utendaji katika baadhi ya nchi zingine, ambazo
alisisitiza kuwa hazina kamati ya mashirika ya umma.
Lakini hili la kujifunza nchi zingine halikuwa muhimu sana,
ila lile la kuunganisha ili kuwe na msemaji mmoja ndilo la msingi zaidi,”
alisisitiza. Alisema kuna kamati ambazo zimeongezeka, ikiwemo inayoshughulikia
Serikali za Mitaa lakini akasema kuwa kesho atafanya mkutano na waandishi wa
habari, kufafanua kwa kina hatua zilizochukuliwa na Bunge kuvunja na kuongeza
baadhi ya kamati.
Dk Bana Kuhusu mabadiliko hayo na athari zake katika Taifa
na dhana ya uwajibikaji, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson
Bana alisema muundo wa taasisi yoyote ikiwamo Bunge, unatokana na majukumu na
changamoto zake. “Kamati za Bunge sio za kibiblia, kwamba hazibadiliki.
Mazingira yanabadilika na jinsi Bunge linavyosimamia
Serikali, linatakiwa kubadilika. “Spika haamui peke yake, ana watu nyuma yake
wanaofanya kazi pamoja na hapa nia ya kufanya hivyo ni kuboresha, hasa utendaji
wa Kamati husika,” alisema Dk Bana na kuongeza inawezekana utendaji wa viongozi
wa Kamati kutoa amri katika mashirika wanayoyasimamia, labda haufuati
utaratibu.
Kuhusu kama Kamati ya PAC yaweza kumudu kazi hiyo, ambapo
Zitto alidai haitaweza, Dk Bana alisema kazi za Kamati ya POAC zinaweza
kufanywa na PAC na kwamba hakuna tatizo kwani mabadiliko hayo yanalenga
kuboresha na kuimarisha dhana kuu ya Bunge kusimamia Serikali.
Wenyeviti wenzake Mwenyekiti wa PAC, John Cheyo (UDP)
alisisitiza Spika aachwe kwa uamuzi wake na kazi iliyopo sasa ni kutekeleza
uamuzi huo. Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Augustine
Mrema (TLP), alisema uamuzi wa Spika, lazima uachwe kama ulivyo.
Hata hivyo, Mrema alielezea hofu aliyonayo kwamba kunaweza
kupitishwa sheria, inayoelekeza kabla ya taarifa ya ukaguzi kufikishwa bungeni,
ipelekwe serikalini na kutafutiwa majibu.
No comments:
Post a Comment