WAFANYABIASHARA katika masoko makubwa ya Manispaa ya Kigoma
Ujiji wamegoma kufanya biashara wakipinga uongozi wa manispaa kuongeza kodi ya
pango ya vibanda na ushuru wa soko kwa asilimia 200.
Akizungumza sokoni hapo, Mwenyekiti wa Soko Kuu la mjini
Kigoma, Yahaya Rukuba alisema wafanyabiashara wamefikia hatua hiyo ya kugoma
kutokana na uongozi wa manispaa kupuuza makubaliano yaliyopo kati yao na kutoa
uamuzi wa upande mmoja katika kupandisha bei hizo.
Mwenyekiti huyo alisema katika mgomo huo, wanapinga kitendo
cha kupandishwa kwa kodi ya pango kutoka Sh 5,000 kwa mwezi na kufikia Sh
15,000 sawa na asilimia 200 huku bei ya ushuru wa kila siku ukipanda kutoka Sh
200 hadi Sh 300.
Alisema awali waliitwa katika kikao na uongozi wa Manispaa
ambao uliwaeleza nia ya kupandisha kodi ya vibanda kutoka Sh 5000 hadi Sh
50,000, jambo ambalo walilipinga na kutokana na hilo walipeana muda ili kufikia
Juni 26, kuwe na kikao cha mwisho katika kukabiliana na bei hizo.
Hata hivyo, alisema kabla ya kufikia tarehe ya kukutana,
walishangazwa na kitendo cha manispaa Juni 25, mwaka huu kubandika matangazo
yanayoelezea kupandishwa kwa bei za pango la vibanda na ushuru wa kila siku
kuanzia Julai mosi mwaka huu.
Mgomo huo, umekuwa na athari kubwa kwa wakazi wa Kigoma
katika kupata mahitaji yao mbalimbali ya kila siku.
Masoko yaliyokumbwa na kadhia hiyo ya mgomo ni Soko Kuu la
mjini Kigoma, Soko la Mwanga na Soko la Buzebazeba ambayo yamekuwa yakihudumia
sehemu kubwa ya wakazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji.
No comments:
Post a Comment