Washindi wa Tuzo ya Kitaifa ya Ubunifu katika Sekta ya Afya. Kutoka kushoto ni Ally Kassinge (Ruangwa), Imelda Ishuza (Makete) na Derick Bakuza (Kasulu).Nyuma yao ni Pape Gaye wa Intra Health International.
HIVI karibuni wilaya za Makete mkoani Njombe na Kasulu
mkoani Kigoma zilipokea ngao na zawadi zilizotolewa mbele ya hadhira ya watu
zaidi ya 200.
Ngao hizo za Tuzo ya Kitaifa ya
Ubunifu katika Sekta ya Afya zilitolewa na Shirika la Intra Health
International. Shirika hili linafanya kazi kwenye nchi 30 zinazoendelea.
Tuzo zilizotolewa na shirika hilo ni za
kutambua ubunifu na juhudi zinazofanywa na wilaya hizo mbili ambazo zimepata
mafanikio makubwa katika kuvutia watumishi wa afya kubakia wakifanya kazi
kwenye wilaya hizo ambazo zina changamoto nyingi. Wilaya za Makete na Kasulu
zinafanana kwa mambo kadhaa.
Zote ziko mbali kutoka miji mikubwa,
ni za vijijini na ziko pembezoni. Isipokuwa zinatofautiana kwa maana kwamba
Makete iko Nyanda za Juu Kusini,na Kasulu iko Magharibi kabisa mwa Tanzania
karibu na mpaka wa Burundi na Congo DRC. Juu ya hayo wilaya hizi zina upungufu
wa wafanyakazi, si wa idara ya afya pekee bali pia wa idara za elimu na kilimo
pia.
Takwimu za shirika la afya
ulimwenguni zinaonesha Tanzania ina wafanyakazi wa afya 1.48 kwa kila watu
1,000. Huu ni wastani wa chini sana ukilinganisha na idadi ya chini iliyowekwa
kimataifa ya wafanyakazi wa afya 2.5 kwa kila watu 1,000 ili kutimiza malengo
ya milenia.
Kwenye nchi yenye kiwango kidogo
namna hiyo cha wafanyakazi wa afya, wilaya za vijijini na pembezoni zinapata
adha zaidi ya upungufu huu. “Wahitimu kutoka vyuoni hawachagui kuja kwenye wilaya
za pembezoni kama hii ya Kasulu kufanya kazi. Wanapendelea kwenda maeneo
maarufu kama Dar e Salaam, Arusha na Mwanza,” anasema Dk. Erick Bakuza, ambaye
ni Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kasulu.
Kati ya watumishi 1,000 ambao Wilaya
ya Kasulu inahitaji, watumishi 350 sawa na asilimia 30 ndiyo waliopo. Matokeo
yake kazi zinawaelemea sana wafanyakazi waliopo kwa kuwa wanalazimika kufanya
kazi kwa saa nyingi zaidi ama kuchukua majukumu yaliyo nje ya uwezo wao
kitaaluma na kiutendaji.
“Katika baadhi ya hospitali na vituo
vya kutolea tiba muuguzi msaidizi anaweza akajikuta akilazimika kufanya kazi
kama muuguzi mkunga kumzalisha mama,” anasema Dk Bakuza. Hapo ndipo ubunifu
unapohitajika.
“Tumekuwa tukifanya uchambuzi mara
kwa mara kutambua ujuzi na stadi ambazo mfanyakazi tuliyenaye anahitaji ili
kuweza kukabiliana na changamoto anazokumbana nazo kutokana na upungufu wa
watumishi wa afya katika vituo vya kutolea tiba. Tunatoa vipaumbele kutoa
mafunzo ya kazini kuwawezesha watumishi kuhudumia wagonjwa,” anasema Dk Bakuza.
Sanjari na mafunzo kazini, Idara ya
Afya ya Wilaya ya Kasulu inadhamini wafanyakazi ili wasome na kupanda madaraja
kwa sharti la kurudi kufanya kazi Kasulu kati ya miaka mitatu hadi mitano
kutegemea na gharama za kozi husika na umuhimu wake.
“Tumeweka pia malipo kwa muda wa
ziada ambao wafanyakazi wanatumia nje ya masaa rasmi. Hatuna uwezo wa kulipa
kila dakika ya muda wa ziada ambao mfanyakazi ametumia kutoa huduma kwa
wagonjwa, lakini tunawalipa kiasi fulani cha pesa kila mwisho wa mwezi pale
wanapokuwa wamefanya kazi zaidi ya muda rasmi,” anaongeza Dk Bakuza.
Ubunifu huo unaongezewa na juhudi
zilizofanyika kujenga nyumba za watumishi kwenye vituo vya kutolea tiba. Ujenzi
wa nyumba za kuishi watumishi ulikuwa pia ni sehemu muhimu ya mikakati ya
Wilaya ya Makete ili kuhakikisha watumishi wanapangiwa kufanya kazi huko
hawaondoki kwa kukosa huduma muhimu.
“Serikali ilitoa fungu kwa wilaya za
pembezoni kujenga nyumba ili kuvutia watumishi. Fedha hizo zilitosha kujenga
nyumba 10, lakini kwa kuhamasisha jamii kuchangia tuliweza kujenga nyumba nane
zaidi katika vituo vya afya vya vijijini. Wilayani hiyo ya Kasulu inalenga
kutafuta suluhisho zaidi. “Tuna maono ya kuanzisha chuo cha kuandaa watumishi
wa kada mbalimbali za tiba hapa wilayani kwetu,” anasema Dk Bakuza.
Kwa upande wa Makete, ilikuwa ni
kawaida wafanyakazi wapya wanaofika wilayani humo, wakiwamo madaktari, wauguzi
na walimu kupata sehemu mbadala ya kufanya kazi na kuhama mara moja wakiachana
na barabara ya mabonde na vumbi inayopanda milimani, na kuikimbia wilaya yenye
umasikini na athari za maambukizi makubwa ya VVU ikibaki na uhitaji mkubwa wa
wafanyakazi.
“Wafanyakazi wengine waliondoka baada
ya kufanya kazi hadi miezi sita bila kupata mshahara kwa kuwa taarifa zao
zilichelewa kuingizwa kwenye orodha ya mishahara ya Serikali. Tumebadili hali
hiyo kabisa, sasa taarifa za watumishi wapya zinapelekwa wizarani mara tu
mtumishi akifika kwenye kituo chake cha kazi,” anasema Imelda Ishuza, ambaye ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya Makete.
Cha ziada ni kuwa Halmashauri ya
Wilaya ya Makete imebuni utaratibu bora wa kuwapandisha watumishi wake vyeo na
madaraja, kinyume na zamani ambapo mtumishi alikaa kwenye daraja moja ama cheo
kimoja kwa muda mrefu hadi akakata tamaa. “Juhudi hizi zimelipa,” anasema
Imelda.
Tangu 2009 hadi 2011 idadi ya nafasi
za kazi zilizowazi katika Halmashauri ya Makete imeshuka kutoka asilimia 77
hadi asilimia 49 na asilimia 97 ya wafanyakazi hawajahama ama kuacha kazi kwa
miaka minne mfululizo. Kwa pamoja Makete na Kasulu zimeweza kutunza wafanyakazi
waliopo, kuongeza morali yao ya kufanya kazi na hata kuajiri wapya kwa
kuboresha mambo yaliyo ndani ya uwezo wao.
Mkurugenzi wa Wilaya Makete hakuweka
lami kwenye barabara ya vumbi inayopanda milimani kama ambavyo imekuwa ikidaiwa
kuwa barabara bora ndizo zenye kuvuta watumishi kwenda maeneo mbalimbali
kufanya kazi. Wala hakusubiri hadi umasikini na Ukimwi ukome kama ambavyo
imekuwa ikielezwa kuwa watumishi wanaogopa kwenda kufanya kazi wilayani humo
kwa hofu ya vitu hivyo.
Badala yake alitumia ubunifu na
kufanya kile kilicho ndani ya uwezo wake. “Tuliamua kujihusisha na yale mambo
ambayo tulikuwa na uwezo wa kuyarekebisha ili kuboresha mazingira ya kufanyia
kazi kwa watumishi,” anasema Ishuza. Kwa kuangalia mbeleni Makete ina mpango wa
kuongeza nyumba za watumishi na kuendelea kuhakikisha watumishi wake wanapanda
vyeo na madaraja kwa wakati.
Juhudi na ubunifu huu wa Makete na
Kasulu ndio ambao ulitunukiwa tuzo za kitaifa za ubunifu katika sekta ya afya
kwenye tuzo zilizodhaminiwa na Intra Health International, shirika lisilo la
kiserikali linaloboresha mifuko ya ajira inayowagusa watumishi wa afya kwenye
nchi 30 zinazoendelea duniani kote.
Bila shaka ubunifu wao katika
kuboresha mazingira ya kufanyia kazi ya watumishi wa afya ni mfano wa kutajwa
na kuigwa na wote wanaotamani kuboresha huduma ya afya.
No comments:
Post a Comment