BAADHI ya maduka ya kuuza dawa muhimu mjini Kigoma yamedaiwa kukiuka
kanuni na utaratibu wa utendaji wake kwa kuuza dawa za kutibu ugonjwa wa
kifua kikuu (TB) kiholela, jambo ambalo ni kosa kisheria.
Uchunguzi
uliofanywa na Asasi ya Mapambano ya Kifua Kikuu na Ukimwi Tanzania
(Mkuta), mkoani Kigoma umebaini kuwepo kwa dawa hizo kwenye maduka ya
dawa baridi ya jumla na rejareja, hivyo kukiuka sheria inayoelekeza dawa
hizo zitolewe bure katika hospitali, vituo vya afya na zahanati
zilizoteuliwa rasmi na mamlaka husika.
Mratibu wa Asasi ya MKUTA
Mkoa wa Kigoma, Maulidi Ntahondi alibainisha ukiukwaji huo wa sheria
akitaja maeoneo husika kuwa ni Kigoma mjini, Bangwe, Gungu na Mwanga na
kwamba maelekezo yanayotolewa na wahudumu wa maduka hayo kuhusu utumiaji
dawa hizo yanatofautiana.
Aliongeza kuwa dawa hizo huuzwa kwa Sh10,000 kwa boksi moja ambapo pia dozi moja ya vidonge ishirini huuzwa kwa Sh4000.
Alipotafutwa
kuzungumzia suala hilo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dk Yakayashi
Macrice alisema kuuza dawa za kutibu TB kwenye maduka hayo binafsi ni
kosa kisheria na kwamba wahusika wanastahili kukamatwa na kufikishwa
mahakamani.
Alisema kuwa dawa hizo zinatolewa na Bohari Kuu ya
Dawa ya Serikali na zinapaswa kutolewa bure kwa wagonjwa wa TB na kwamba
ni lazima zitolewe katika vituo vya afya, hospitali au kwenye zahanati
maalumu zilizoteuliwa kulingana na jiografia ya wilaya husika zikiwa na
wataalamu wa afya.
Alimuagiza Mfamasia Mkuu wa Mkoa wa Kigoma
kuhakikisha kuwa wote wanaouza dawa hizo kwenye maduka binasfi
wanakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.
Baadhi ya watumishi wa
maduka binafsi ya dawa yanayouza dawa hizo bila kufafanua walieleza
kuwa dawa hizo za TB huuzwa kwa kuwa zina matumizi tofauti na kutibu
ugonjwa huo
No comments:
Post a Comment