Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, June 6, 2012

Waziri kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe akizungumza na waandishi wa habari vipaumbele vya Kambi ya Upinzani Bungeni katika bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013

Waziri kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe 



KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), imeunda tume ndogo kuchunguza uuzwaji wa Kiwanja Namba 10 ambacho kilikuwa kinamilikiwa na Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC), kabla ya kuuzwa katika mazingira tata kwa Kampuni ya Mohamed Enterprises (MeTL).

Kiwanja hicho ni miongoni mwa sababu zilizomng’oa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo baada ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuonyesha jinsi alivyoshiriki kwa namna moja au nyingine katika uuzaji wa kiwanja hicho huku akiivunja Bodi ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) ili kuficha tuhuma hizo.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe alisema kutokana na mgogoro wa uuzaji wa kiwanja hicho, wamepokea ripoti maalumu kutoka CHC ambayo imeonyesha uuzaji wa kiwanja hicho pamoja na mali za Serikali zilizokuwa zinamilikiwa na NMC.


Zitto alisema kutokana na utata huo huku mali za NMC zikiwa hazijulikani vema, kamati yake imeunda tume ndogo kuchunguza suala hilo, ili waweze kuwasilisha taarifa bungeni na kutoa uamuzi na kuishauri Serikali kuhusu suala hilo.


“Suala la uuzaji wa Kiwanja Namba 10 ni nyeti sana, yaani bado ngoma nzito. Linahitaji umakini wa hali ya juu ili kulimaliza. Kutokana na hali hiyo, tumeamua kuunda kamati ndogo ambayo itafanya uchunguzi na kutoa taarifa bungeni ili tuweze kuchukua hatua,” alisema Zitto.

Alisema mpaka sasa, NMC bado iko hai, ina mkurugenzi ambaye analipwa mshahara kutokana na pango la majengo yake, lakini cha kushangaza hawana kitabu cha benki kinachoonyesha kiasi cha fedha zilizopo ambazo zimetokana na pango hilo.

Mwenyekiti huyo wa POAC, alisema kutokana na hali hiyo kuna nafasi kubwa ya kuwapo kwa wajanja ambao wamerithi mali za NMC bila ya Serikali kujua jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa kuna ubabaishaji ndani yake.


Alisema mbali na suala hilo, pia majengo ya NMC yamepangishwa kwa kampuni ya Noble Azania kwa zaidi ya miaka 20 sasa lakini hawajawahi kulipa kodi na wala hawajulikani wanaishi humo kwa kufuata utaratibu upi, jambo ambalo limewafanya waamue kutembelea mali hizo ikiwa pamoja na kukagua vinu.

“Kamati inataka kujua mali zilizoachwa na NMC kabla ya kubinafsishwa ili tuweze kubaini kuna nini, lakini taarifa tulizonazo zinaonyesha kuwa kuna viwanja vingi nchi nzima, kuna mashine na vinu vilivyokuwa vinatumika kwa ajili ya usagishaji, lakini mpaka sasa havijulikani vilipo, jambo ambalo limetufanya tutembelee mali hizo,” aliongeza.

Alisema kuna uhamisho wa mali nyingi kwenda kwa kampuni binafsi na mashirika ya umma bila ya kufuata taratibu za kisheria, hivyo wameamua kufanya hivyo ili kuhakikisha mali zote za umma zinatambulika, ikiwa ni pamoja na kuishauri Serikali kuwachukulia hatua watu au kampuni zinazomiliki mali hizo kinyume na taratibu.


Zitto alisema tayari wameanza na NMC lakini, watafuatilia kampuni zote ambazo zilibinafsishwa na Serikali miaka iliyopita ili waweze kuangalia uhalali wa ubinafsishaji huo, pamoja na hatua stahiki kwa kampuni zilizoshindwa kufuata taratibu za kisheria.


“Mpaka sasa taarifa maalumu tunazo, ila tunachotaka kujua ni kuhakikisha kuwa NMC ilikuwa na mali gani na ziko wapi, ili jamii na Serikali kwa ujumla waweze kujua kinachoendelea kuhusu suala hilo,” alisema.


Kiwanja Namba 10

Sakata la Kiwanja namba 10 kilichouzwa MeTL, lilianza kunukia Oktoba 10 mwaka jana, baada ya Mkulo kuamua kuvunja ghafla bodi ya CHC kabla haijamaliza muda wake mnamo Desemba 31.
Awali, bodi hiyo ilikuwa imalize muda wake Juni 30, 2011, lakini Mkulo alitumia mamlaka yake kuongeza muda hadi Desemba 31. Hata hivyo, ghafla alibadili uamuzi huo wakati bodi hiyo ilipaswa kupokea ripoti ya uchunguzi wa kiwanja hicho.

Hatua hiyo iliibua utata kwani badala ya ripoti hiyo kukabidhiwa bodi ya CHC sasa ilipaswa kwenda kwa Mkulo mwenyewe wakati uchunguzi ulikuwa ukimhusisha pia.


Hatua hiyo ya Mkulo ilikuja siku chache baada ya kujibu maswali ya CAG kuhusu alivyoshiriki mchakato wa kuuzwa kwa kiwanja hicho kama ilivyokuwa imeonyeshwa katika uchunguzi wa Kampuni ya Ernst & Young, kubaini tuhuma zilizokuwa zimetolewa na POAC.


Katika hatua nyingine, Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangwala, amesusa kujadili bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kutokana na vitabu kuchelewa kuwafikia wajumbe wa Kamati ya Huduma za Jamii.


Baada ya Dk Kigwangwala kususa kushiriki, wabunge wengine walimsihi kuendelea ili aongeze nguvu ya wabunge waliokuwa hawaridhishwi na bajeti hiyo, lakini alishikilia msimamo wake.


Mbunge huyo alisema ataendeleza hatua yake hiyo kwenye kikao cha muhtasari Jumatatu mjini Dodoma.

“Nimesusa na kumtaka katibu wa kamati aingize kwenye kumbukumbu rasmi kuwa nimerudisha vitabu na sitajadili mpaka tutakapopewa muda wa kutosha wa kusoma kwanza na kuchambua na siyo kulipua lipua tu,” alisema Dk Kigwangwala na kuongeza:

“Ijumaa kamati yote iliandika barua kwa Spika ikipendekeza tuongezewe wiki moja barua hiyo haijajibiwa mpaka leo.”

No comments: