MTOTO wa kijiji cha Kigadye, Kasulu mkoani hapa, Obedi
Manase (8), amepoteza maisha baada ya kulipukiwa na bomu la kutupa kwa mkono
alilokuwa akichezea na watoto wenzake wanne ambao wamejeruhiwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Fraiser Kashai alisema jana mjini
hapa kuwa ajali hiyo ilitokea mwanzoni mwa wiki kijijini hapo.
Alisema Obedi ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza wa
shule ya msingi ya Kidadye na wenzake wanne ambao wamelazwa katika hospitali ya
misheni ya kijiji cha Shunga ambao hali zao zinaendelea vizuri, walikuwa
wakichezea bomu hilo
bila kulitambua.
Alitaja waliojeruhiwa kuwa ni Tuju Seluke (7) aliyejeruhiwa
tumboni, Sarah Manase (6) pajani, Enjo Seluke (4) sikioni na Isaka Yohana (4)
jichoni.
Kamanda Kashai alisema uchunguzi uliofanywa na Jeshi hilo, ulibaini kuwa watoto hao waliokota bomu hilo lililokuwa limefichwa kwenye maua na baba mdogo wa marehemu aitwaye Ayubu
James ambaye ametoroka na juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Kijiji hicho ambacho kiko mpakani na Burundi, kimekuwa na mwingiliano
mkubwa na watu kutoka nchi hiyo na kimekuwa kikumbwa na matukio mbalimbali ya
milipuko.
Enzi za vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, kilikuwa
moja ya vijiji ambavyo waasi wa nchi hiyo walikuwa wakikimbilia kujificha dhidi
ya mashambulizi ya majeshi ya Serikali wakati huo.
Katika matukio mengine, Kamanda Kashai alisema jeshi lake kwa
kushirikiana na Idara ya Uhamiaji Mkoa, imekamata wahamiaji haramu 52 kutoka
nchi za Maziwa Makuu ambao wamekuwa wakiishi kwenye vijiji mkoani hapa.
Alisema katika operesheni hiyo iliyofanyika kuanzia Mei 25
hadi Juni 5, wengi wa wahamiaji hao wanaotoka Burundi
na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), walikuwa wakijishughulisha na uvuvi
katika mwambao wa Ziwa Tanganyika.
No comments:
Post a Comment