HALMASHAURI ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma imeingia
mkataba wa miaka mitatu na kuipatia Kampuni ya Mawalla Trust Ltd ya mkoani
Arusha, hekta 157,510 za ardhi kwa ajili ya mradi wa uwekezaji wa ranchi ya wanyama.
Utiaji saini huo ambao ulifanyika mbele ya wajumbe wa Baraza
la Madiwani wa Halmashauri hiyo katika uwekezaji huo utaiwezesha halmashauri
kupata Sh milioni 440 kila mwaka kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii na
kuhifadhi rasilimali za eneo hilo.
Akisoma mkataba huo mbele ya wajumbe wa kikao cha Baraza la
Madiwani kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Kasulu, Mwanasheria
wa Halmashauri, Alphonce Sebukoto alisema uwekezaji huo unalenga kuendeleza
maliasili na uchumi wa wilaya hiyo.
Alisema kuwa miongoni mwa shughuli zitakazofanyika kwa
mujibu wa mkataba huo ni pamoja na utalii wa uwindaji wanyama, kuangalia
wanyama, upigaji picha, uendeshaji wa mahoteli na kambi za utalii.
Akizungumzia uwekezaji huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji
wa Kampuni hiyo, Adam Mawalla, wakili wa Kampuni ya Mawalla Trust Limited,
Wilbright Mamkwe alisema kuwa uwekezaji unaofanyika unazingatia kuwafanya wanyama
kuwa rafiki wa binadamu.
Alisema kampuni yake kabla ya kufanya uwekezaji huo
imevifanyia vijiji vinavyozunguka ranchi
hiyo mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuondoa migogoro na wananchi
wanaoishi katika vijiji hivyo na kuwapa elimu kuhusu uwekezaji.
Alisema kuwa kampuni hiyo inayomilikiwa kwa asilimia 100 na
Watanzania pamoja na mambo mengine, imelenga kuhakikisha wananchi wanaoishi
karibu na eneo hilo
la uwekezaji, wananufaika.
No comments:
Post a Comment