USIMAMIZI dhaifu wa sheria za utunzaji na uhifadhi wa
mazingira, umetajwa kuwa kikwazo katika mradi wa maendeleo ya Bonde la Ziwa
Tanganyika na kusababisha kushindwa kuchukua hatua dhidi ya wanaoharibu
mazingira.
Meneja wa Mradi huo, Hawa Mshamu alisema hayo jana katika
ziara ya kutembelea baadhi ya maeneo ya mradi baada ya mkutano wa siku moja wa
wadau kupeana taarifa ya hali ya maendeleo ya mradi huo.
Alikuwa akijibu baadhi ya maswali ya wajumbe wa ziara hiyo
waliotaka kujua uongozi wa mradi unachukua hatua gani kwa watu wanaokaidi
kutekeleza mradi au wanaoharibu mazingira.
Alisema kazi kubwa ya mradi ni kutoa elimu kwa jamii ya nini
kifanyike kwa manufaa ya siku za baadaye pamoja na kusimamia miradi mbalimbali
ya utunzaji na uhifadhi mazingira, ikiwemo upandaji miti na miradi ya
kujiingizia kipato kwa jamii katika baadhi ya vijiji.
Akizungumza katika mkutano huo wa siku moja, Mkurugenzi wa
Mazingira wa Mamlaka ya Bonde la Ziwa Tanganyika (LTA), Gabriel Hakizimana
alisema kuwa yapo mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza kwa mradi ingawa zipo
changamoto ambazo bado zinatakiwa kufanyiwa kazi zaidi.
Hakizimana alisema kikubwa zaidi elimu na uhamasishaji jamii
unatakiwa kufanywa kwa nguvu kubwa ili kuifanya jamii itambue umuhimu wa
utunzaji na uhifadhi wa bonde hilo kwa kipindi kirefu kijacho na kuvitaka
vyombo vya habari kushiriki katika mkakati huo.
Alisema Ziwa Tanganyika ni urithi wa dunia likiwa na zaidi
ya aina 600 za viumbe ambapo kati yake, 200 havipatikani mahali popote zaidi ya
ndani ya ziwa hilo.
Kutokana na umuhimu huo, aliitaka nchi na jamii inayozunguka
ziwa hilo, kulitunza kwa hali na mali. Akifungua mkutano huo Mkuu Wilaya
Kigoma, Ramadhani Maneno alisema wananchi wanapaswa kulifanya suala la uhifadhi
na utunzaji mazingira ya Bonde la Ziwa Tanganyika kuwa sehemu ya maisha yao kutokana
na umuhimu wa ziwa hilo.
No comments:
Post a Comment