Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila
(NCCR Mageuzi)
MBUNGE wa Nkasi Kaskazini, Mohamed Keisy (CCM) amesema
wabunge pamoja na taasisi ya Bunge vinanuka rushwa na kutaka Chama cha Wabunge
Wanaopambana na Rushwa (APNAC), kuchukua hatua za haraka kurekebisha suala hilo.
Akizungumza jana katika semina ya wabunge ambao ni wanachama
wa APNAC, Keisy alisema kitendo cha wabunge kunuka rushwa sio kizuri hata
kidogo kwani watakosa nguvu za kukemea suala hilo.
“Mwenyekiti wabunge wananuka rushwa na Bunge limegubikwa na
fununu za rushwa ambazo ni nyingi, hivi tufanyeje kwenye suala hili? alihoji
mbunge huyo.
Wabunge ambao ni wanachama wa APNAC waliandaliwa semina hiyo
na asasi isiyo ya kiserikali ya Policy Forum kwa ajili ya kuzindua ripoti
kuhusu ushindani wa kodi ndani ya Afrika Mashariki hususani upotevu wa mapato nchini
katika masuala ya kodi.
Mbunge huyo pia katika mchango wake, alitaka watu wajitume
kufanya kazi badala ya kuilaumu Serikali kuwa maisha ni magumu wakati wananchi
wengi hasa wa mwambao wa Pwani hawataki kufanya kazi.
Wakati huo huo, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila
(NCCR Mageuzi) ameliambia gazeti hili jana kuwa ameshaandika barua ya kujiuzulu
ujumbe wa Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC) kutokana na kamati hiyo
kunuka rushwa.
Kafulila alisema ameandika barua hiyo Ijumaa wiki iliyopita
na kuiwasilisha kwa Spika wakiwa bado jijini Dar es Salaam kutimiza azma yake
ya kujiondoa kwenye kamati hiyo ambayo alisema haina maadili hata kidogo.
“Mle ndani ya kamati wala rushwa ni wengi, suala ni
kuzidiana tu na hata siku ya tukio ambayo mmoja wetu alikamatwa, kuna mjumbe
mwingine (jina tunalo) alichelewa tu kwenye foleni naye alikuwa ameahidiwa
kwenda kuchukua fedha hizo,” alidai Kafulila.
No comments:
Post a Comment