Paul Chizi, aliyekuwa Mkurugenzi wa ATCL |
Ndege iliyodindoka ikitoka Kigoma kwenda Tabora
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ametengua uteuzi
wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Paul Chizi na
kusimamisha kazi wakurugenzi wengine wanne wa kampuni hiyo.
Aidha, amemteua Kapteni Lusajo Lazaro, kuwa Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji wa Kampuni hiyo tangu jana
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Wizara hiyo
jana, ilisema uteuzi huo umetenguliwa baada ya kubainika kuwa ulifanyika bila
kufuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Sheria ya mwaka 2002 na Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka
2003, inaelekeza bayana kuwa kama uteuzi
utakuwa umefanyika kwa kukiuka sheria, utatenguliwa mara moja,” ilieleza
taarifa hiyo. Wakurugenzi wengine waliosimamishwa kazi ni pamoja na Kaimu
Mkurugenzi wa Uhandisi, John Ringo; Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Justus Bashara;
Mwanasheria wa ATCL, Amini Mziray na Kaimu Mkurugenzi wa Biashara, Josephat
Kagirwa.
Chizi aliteuliwa kukaimu nafasi hiyo Agosti 6 mwaka jana,
baada ya aliyekuwa Mkurugenzi wake, David Mattaka kujiuzulu na baadaye
kufikishwa mahakamani kwa kutumia vibaya madaraka na kuisababishia hasara
kampuni hiyo.
Baada ya Chizi kushika nafasi hiyo, kampuni hiyo imekuwa
ikiongeza idadi ya ndege na hivi karibuni ilizindua tovuti ikiwa ni katika
jitihada za kutangaza huduma zake kwa wadau wa ndani na nje ya nchi. Kampuni
hiyo imekuwa katika matatizo kadhaa ambapo hivi karibuni ndege yake aina ya
Dash 8 Q300 ilishindwa kuruka na kuingia porini ikiwa na abiria 39 katika
uwanja wa ndege wa Kigoma.
Ndege hiyo ilikuwa ikitoka Kigoma kwenda Tabora na baadaye
Dar es Salaam na ilivunjika vipande kabla ya kikosi cha Zimamoto kufika na
kudhibiti uwezekano wa kuteketea kwa moto.
Sababu za kushindwa kuruka, zilielezwa kuwa ni kutokana na
matope yaliyokuwa kwenye njia ya ndege kuruka na kuifanya ipoteze mwelekeo.
Hata hivyo, baada ya kukaa muda bila ndege, hivi karibuni
kampuni hiyo ilikodi ndege nyingine kutoka Dubai Boeing 737-500 ambayo imeanza
kazi.
Mbali na kufanya kazi ikiwa na ndege moja, kampuni hiyo pia
imekuwa ikijiendesha kwa ruzuku ya Serikali baada ya kukaa kwa muda mrefu bila
kufanya biashara huku ikiingia gharama za kulipa wafanyakazi na nyingine za
uendeshaji.
No comments:
Post a Comment