SERIKALI imevitaka Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Nchini
(VETA) kuwa wazi na kuweka matangazo kwenye vyombo vya habari kuhusiana
na udahili mpya wa wanafunzi kujiunga na vyuo hivyo ili kuwafanya watu
wengi zaidi kujua taratibu za kujiunga na vyuo hivyo.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo amesema
hayo alipokuwa akizungumza na wakufunzi na watumishi wa Chuo cha VETA
Kigoma alipokuwa kwenye ziara ya siku mbili mkoani humo kutembelea
taasisi zilizo chini ya Wizara yake ambapo sambamba na hilo ametaka vyuo
hivyo kutangaza sifa za wanafunzi wanaostahili kujiunga navyo.
Mulugo amesema kuwa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi ambao
wanaeleza kutaka kutumia fursa ya kupeleka watoto wao kupata mafunzo
kutoka katika vyuo hivyo lakini taratibu za kujiunga na sifa za wanachuo
limekuwa tatizo kubwa kwao.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi ametangaza kutafuta popote walipo walimu zaidi ya 100 ambao
wamepangiwa kufundisha mkoani Kigoma lakini hawakuripoti katika vituo
vyao na badala yake kufanya ujanja na kubadilishiwa mikoa.
Awali Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Kigoma, Alban Kisomba amesema kuwa
chuo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mkoa kukosa
viwanda jambo linalowafanya wanafunzi kushindwa kufanya mafunzo kwa
vitendo.
Ili kukabiliana na hali hiyo alisema kuwa wamelazimika kuwapeleka
wanafunzi wa ufundi katika chuo hicho kwenye viwanda vilivyopo nje ya
mkoa vinavyoendana na fani zao jambo ambalo ni gharama kubwa kwa
wanafunzi na uongozi wa chuo.
No comments:
Post a Comment