MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA), Mkoa Kigoma imewatahadharisha
wafanyabiashara mkoani hapa kuachana na vitendo vya kuchezea mashine
maalumu za kutoa risiti.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa TRA Mkoa wa Kigoma, Augustino Mukandara.
Amesema katika mkutano wa siku moja wa Elimu kwa Walipa Kodi
uliowajumuisha wafanyabiashara wa Manispaa ya Kigoma Ujiji kuwa kitendo
cha wafanyabiashara kuchezea mashine hizo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria.
Mukandara aliwaambia wafanyabishara hao kulipa kodi kwa hiari na kwa
kuzingatia sheria ili kuiwezesha mamlaka ya mapato kukusanya mapato ya
kutosha na kuiwezesha Serikali kuwa na mapato ya kutosha kugharimia
shughuli mbalimbali za maendeleo nchini.
Aidha Meneja huyo wa TRA Mkoa wa Kigoma ametoa wito kwa
wafanyabiashara mkoani Kigoma kutoa taarifa mapema kwa mawakala
waliowasambazia mashine hizo na kuandika muda ambao mashine husika
iliacha kufanya kazi ili kuepuka usumbufu usio wa lazima wa kisheria kwa
mfanyabiashara kupewa adhabu.
Kwa upande wao wafanyabiashara katika Manispaa ya Kigoma Ujiji
wamesema kuwa mkutano huo wa siku moja umekuwa na manufaa makubwa sana
kutokana na kupata maelezo na maelekezo sahihi juu ya utumiaji wa
mashine za risiti na kurudishwa kwa kodi ya ongezeko la thamani VAT.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Bernard Sadala alisema kuwa uwepo wa
mashine hizo utawezesha Serikali kupitia TRA kukusanya kodi sahihi
inayopaswa kulipwa na wafanyabishara.
No comments:
Post a Comment