NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo ameamuru
kukamatwa na kushitakiwa kwa wakuu wa shule 10 za sekondari mjini Kigoma
Ujiji ambao wamebainika kuruhusu wanafunzi 391 waliofeli mitihani yao
ya kumaliza elimu ya msingi, kuendelea na masomo ya sekondari.
Mulugo alisema hayo kwa nyakati tofauti akiwa katika ziara ya siku
mbili mkoani hapa na kuongeza kuwa baada ya hatua ya awali ya kuwavua
madaraka ya ukuu wa shule na uchunguzi kufanywa na tume mbalimbali,
imethibitika kuwa wakuu hao walihusika na vitendo hivyo.
Alisema walifanya vitendo hivyo kinyume na Sheria ya Elimu namba 25
ya mwaka 1978 na marekebisho yake ya mwaka 2002, huku wakijua vitendo
hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria za uendeshaji shule za sekondari.
Akizungumza katika sekondari ya Kasingirima, Naibu Waziri alisema kuwavua madaraka ilikuwa ni hatua ya awali ya kinidhamu.
Baada ya hapo, kinachofuata ni kuchukuliwa hatua za kisheria kwa
sababu vitendo vilivyofanyika vya kuwadahili wanafunzi wasio na sifa
kuendelea na masomo ya sekondari katika mfumo rasmi wa Serikali, ni
kinyume cha sheria.
"Hapo kwa haraka haraka kuna makosa mawili tayari yametendeka; moja
ni kughushi nyaraka halali za Serikali na kuwaingiza wanafunzi hao,
lakini la pili ni vitendo vya rushwa ambavyo vinaonekana kutendeka
katika kuwaingiza wanafunzi hao," alidai.
Katika ziara yake jana mjini Kigoma, Mulugo alitembelea shule tano
za sekondari zinazotuhumiwa kuhusika na kadhia hiyo ambazo ni
Kasingirima, Mwananchi, Katubuka, Masanga na Mlole. Pia alitembelea
Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) na jioni alikwenda katika mkutano wa
majumuisho na viongozi mbalimbali.
Sambamba na ziara katika maeneo hayo pia, Mulugo anatarajia kuwa na
mkutano wa hadhara katika viwanja vya Mwanga Centre ambapo pamoja na
mambo mengine alipanga kuwaeleza wazazi madhara ya kuwaingiza katika
mfumo rasmi wanafunzi waliofeli mitihani ya kumaliza elimu ya msingi.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kasingirima, Nkanuliye Hamisi, alikanusha
kuhusika na kuwaingiza wanafunzi na kujipatia fedha akidai kuwa
alishangazwa na kuwapo kwa wanafunzi hao baada ya kufanyika ukaguzi
kutoka nje na kuwa jambo hilo lilifanywa kinyemela kwa wanafunzi kuingia
bila kusajiliwa.
Hata hivyo, Elisha Zilikana ambaye ni Mkuu wa Shule ya Sekondari
Mwananchi, alikiri kuhusika kuingiza sekondari wanafunzi waliofeli
mitihani yao ya darasa la saba akidai kuwa jambo hilo lilifanyika
kutokana na huruma kwa watu wanaomzunguka huku akiomba kupewa msamaha
kutokana na jambo hilo.
Mwishoni mwa mwaka jana, Ofisi ya Mkaguzi wa Sekondari Kanda ya Ziwa
Magharibi ilifanya ukaguzi na kugundua uwepo wa wanafunzi 391
wanaoendelea na masomo ya sekondari wakati walifeli masomo yao ya shule
za msingi.
Shule hizo za sekondari zilizokumbwa na kadhia hiyo ni pamoja na
Mwananchi, Kasingirima, Rusimbi, Kitongoni, Katubuka, Buteko, Wakulima,
Mlole na Masanga ambapo wanafunzi waliokuwa wakisoma katika shule hizo,
walilazimika kusitisha na masomo.
No comments:
Post a Comment