SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) linatarajia kujenga kituo
cha kisasa cha mabasi chenye hadhi ya kimataifa yaendayo nje ya mkoa
katika eneo la Mwandiga, Kigoma Vijijini.
Meneja Mipango na Uwekezaji wa Shirika hilo, Mseli Abdallah alieleza hayo alipokuwa akitoa taarifa kwenye kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo mjini Kigoma jana.
Abdallah alisema kuwa mradi huo unatarajia kuanza kutekelezwa kuanzia Julai Mosi mwaka huu kwa mujibu wa mpango kazi wa mradi huo baada ya kumalizika kwa taratibu mbalimbali ikiwemo fidia na upembuzi wa kina wa mradi.
Alisema kuwa katika utekelezaji wa mradi huo kwa njia ya ubia NSSF itatoa fedha kwa ajili ya gharama za ujenzi huku Halmashauri ya wilaya Kigoma ikitoa ardhi na kulipa fidia kwa watu watakaohamishwa kupisha mradi huo.
Sambamba na hilo meneja huyo alisema kuwa shirika lake pia litasimamia mwanzo hadi mwisho wa ujenzi wa mradi huo na baada ya hapo kitaundwa chombo maalumu kwa ajili ya uendeshaji wa mradi.
Hata hivyo, alisema kuwa kwa sasa thamani halisi ya mradi haijajulikana na hilo litajulikana baada ya kufanyika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa michoro Aprili mwaka huu.
Wakizungumzia kuhusu mradi huo wajumbe wa baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya Kigoma walisema kuwa kutekelezwa kwa mradi huo itakuwa ukombozi na maendeleo makubwa kwa halmashauri yao.
Dominick Kweka, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kigoma alisema kuwa kutekelezwa kwa mradi huo pamoja na kuchangia kuiingizia halmashauri mapato lakini pia utakuwa chachu katika maendelo ya mkoa.
Kweka alisema kuwa hawana budi kuunga mkono kwa dhati utekelezaji wa mradi huo kwani kwa hali ya sasa ya halmashauri pamoja na nia ya kufanya jambo hilo lakini haina fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ikiwa peke yake.
Naye Mkuu wa Wilaya Kigoma, John Mongela alisema kuwa mradi huo utasaidia kuondoa msongamano wa magari mjini Kigoma katika miaka ijayo lakini utakuwa chachu katika kuharakisha maaendeleo ya mkoa.
No comments:
Post a Comment