Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Monday, January 30, 2012

Mkulima afa kwa kunyweshwa tindikali Kigoma

MKULIMA wa kijiji cha Kibwigwa kata ya Mwayaya wilayani Kasulu, Gaudence Kibiriti, ameuawa na wananchi wa kijiji hicho kwa kunyweshwa tindikali aina ya Caustic.

Wananchi hao walifanya mauaji hayo mwanzoni mwa wiki hii wakimtuhumu kumkingia kifua baba yake, anayetuhumiwa kufanya vitendo vya kishirikina.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa Kigoma, Fraiser Kashai, aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana, kwamba baada ya kumwua mkulima huyo, wananchi hao walimshambulia baba yake mzazi, Kibiriti Shingwa, na kumjeruhi kwa kummwagia tindikali hiyo pia.


Alisema awali wananchi hao walivamia nyumbani kwa Gaudence na kurusha mawe juu ya paa la nyumba yake.


Baada ya hali hiyo, Gaudence alitoka nje ili kunusuru maisha yake, ndipo wananchi walipomkamata na kumnywesha tindikali hiyo na nyingine kummwagia mwilini na

kumsababishia kifo hicho.

Katika tafrani hiyo kwa mujibu wa Kamanda Kashai, wanakijiji hao walivamia shamba la migomba la marehemu lenye ukubwa wa robo heka na kufyeka mazao yote.


Pia waliharibu nyumba zake mbili na kumjeruhi Shingwa sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kummwagia tindikali.


Alisema majeruhi amelazwa katika Hospitali ya Misheni ya Heri katika tarafa ya Manyovu, Kasulu kwa matibabu na juhudi za Polisi kuwatafuta watuhumiwa zinaendelea na hadi jana hakuna mtu ambaye alishakamatwa.


Katika tukio lingine, Kamanda Kashai alisema Polisi inamshikilia mkulima wa kijiji cha Bweranka, Kasulu, Ngenzi Maliyatabu, kwa tuhuma za kukutwa na vipande 13 vya meno ya tembo vikiwa kwenye magunia ya mchele.


Mtuhumiwa alikamatwa juzi Kasulu akiwa kwenye basi la Adventure lililokuwa likitoka Mpanda, Rukwa kuja hapa na alikamatwa baada ya Polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema.


Tukio la mkulima huyo kunyweshwa na kumwagiwa tindikali limekuja siku chache baada ya mfanyabiashara wa Zanzibar Alvind Asawla na mkewe Bimal, kupigwa risasi na kumwagiwa tindikali kwa sababu ambazo awali zilielezwa ni kutokana na kuuza pombe.


Hata hivyo, Jeshi la Polisi Zanzibar lilisema mashambulizi hayo yaliyofanywa na watu wasiojulikana, hayahusiani na uuzaji pombe, bali ni ujambazi uliofanywa na watu waliokuwa wanataka fedha za mauzo ya mfanyabiashara huyo.


Wanafamilia hao walivamiwa Jumatano wiki jana, wakiwa njiani kurudi nyumbani. Bimal alishambuliwa na risasi tumboni na kumwagiwa tindikali huku akiwa na ujauzito wa miezi minne.


Mumewe alipigwa risasi ya uso iliyotokea upande wa pili shingoni na wote walijeruhiwa na wamelazwa hospitalini Dar es Salaam.


Septemba mwaka jana mfuasi wa CCM, Mussa Tesha (25), alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana, wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimboni Igunga, Tabora.


Baada ya tukio hilo, Tesha alipelekwa Hospitali ya Igunga na baadaye Muhimbili Dar es Salaam na kisha India, ambako alipata matibabu zaidi na hivi sasa amerejea nchini akiwa na makovu makubwa usoni.

No comments: