MFUKO wa Taifa wa
Bima ya Afya (NHIF) umesema kuanzia mwakani madaktari bingwa wasio na
vituo maalumu, watapelekwa kila mkoa nchini ikiwa ni utekelezaji wa moja
ya mikakati ya Mfuko huo ya kuboresha huduma za afya kwa wanachama
wake.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Emmanuel Humba, alisema hayo jana
katika kikao cha wadau wa mkoani hapa na kusema uboreshaji huduma ndio
msingi wa sasa wa Mfuko huo.
Humba alisema lengo la mpango huo ni kusaidia wanachama kupata
huduma za madaktari bingwa kutoka maeneo yao, hasa wa vijijini, ili
kupunguza gharama na muda wa kusafirisha wagonjwa nje ya mkoa au nchi.
Alisema kuimarishwa kwa utoaji huduma wa Mfuko huo kutachangia
kuhamasisha wanachama wenye sifa za kujiunga na Mfuko huo kuongezeka,
lakini pia kufanya Watanzania wengi kunufaika na huduma za Mfuko huo.
Sambamba na hilo, Humba alitaka uhamasishaji ufanywe kwa wananchi wa
vijijini ili wajiunge na mifuko ya afya ya jamii, kwani kwa sasa
imekuwa na mchango mkubwa katika kusaidia huduma za matibabu vijijini.
Mjumbe wa Bodi ya Mfuko huo, Gratian Mukoba, alitaka watoa huduma
mkoani hapa kutumia fursa ya mikopo ya vifaa tiba na ya ukarabati,
ambayo Bodi iliidhinisha, ili vituo vya matibabu viwezeshwe kwa kuwa na
vifaa vya kisasa vya uchunguzi na maabara.
Akifungua kikao cha wadau Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya,
alisema anasikitishwa na uchangiaji duni wa jamii kwenye Mfuko na alitoa
mwito kwa kila kiongozi kwa nafasi yake, atafakari hilo na kuja na
mkakati wa kuhakikisha hali inabadilika na wananchi wengi zaidi
wanajiunga.
No comments:
Post a Comment