Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, February 8, 2012

Kigoma wagumu kutoa taarifa za rushwa

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kigoma, imesema mwamko mdogo wa wananchi kujitokeza kutoa taarifa za vitendo mbalimbali vya rushwa katika jamii ni changamoto kubwa kwao inayokwamisha mkakati wa kupambana na vitendo
hivyo mkoani humo.

Mwanasheria wa Takukuru Mkoa wa Kigoma, Sweethbert Rwegasira alisema hayo wakati wa uzinduzi wa mradi wa utoaji wa elimu juu ya madhara ya rushwa kwa jamii unaoendeshwa na Shirika lisilo la kiserikali la Kioo katika kata nane za Wilaya ya Kigoma Vijijini kwa ufadhili wa Ubalozi wa Finland nchini.


Alisema vitendo vingi vya utoaji na upokeaji rushwa vinahusisha jamii kwa hiyo ili kupata uthibitisho wa vitendo hivyo, jamii inapaswa ishiriki kikamilifu kutoa taarifa kwa taasisi hiyo ili kuchukua hatua.


Alisema bila kupata msaada wa jamii katika kutoa taarifa kwao, Takukuru haiwezi kufanya lolote kwa sababu sehemu kubwa ya vitendo hivyo vinafanywa kwa makubaliano baina ya pande mbili, mtoaji na mpokeaji.


Alisema kuwepo kwa mradi huo kutasaidia taasisi yake katika kutekeleza mkakati wa utoaji elimu kwa jamii kuchukia vitendo vya rushwa, lakini pia wasaidie kutoa taarifa juu ya vitendo hivyo.


Kwa upande wake, Mratibu wa Shirika la Kioo, Edward Simon alisema Sh milioni 93 zinatarajia kutumika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ambao kwa kiwango kikubwa unalenga kuiwezesha jamii kujua madhara ya kutoa na kupokea rushwa katika utoaji huduma kwa jamii.

No comments: