Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Thursday, February 9, 2012

Mkakati kusafisha Kigoma Ujiji waanza

Manispaa ya Kigoma Ujiji

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, imeanza utekelezaji wa mkakati wa kuuweka
mji wa Kigoma Ujiji katika mazingira safi baada ya vikundi vya uzoaji taka kuanza kufanya
kazi.

Ofisa Afya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Ernest Nkonyozi alisema hayo juzi wakati akipokea vifaa vya kufanya usafi vilivyotolewa na Mradi wa Maendeleo ya Bonde la Ziwa Tanganyika. Aliongeza kuwa mkakati huo unakusudia kuifanya manispaa hiyo kuwa miongoni mwa manispaa zitakazoongoza kwa usafi.


Pamoja na hilo, Nkonyozi alisema kuwa ofisi yake imeongeza magari ya kuzolea taka kutoka mawili yaliyokuwa awali na kufikia matatu huku magari mawili yakiwa njiani kuongeza nguvu katika mkakati huo.


Kwa sasa alisema kuwa Manispaa ya Kigoma Ujiji bado inakabiliwa na hali mbaya ya taka kutokana na kiasi kikubwa cha taka kinachozalishwa kushindwa kuzolewa. Kwa sasa tani 120 za taka huzalishwa kwa mwezi wakati uwezo wa manispaa hiyo kuzoa taka hizo ni tani 46 ambazo ni chini ya nusu ya kiwango kinachozalishwa.


Nkonyozi alisema tayari juhudi za kuzoa taka zinaonekana kuongezeka kutokana na kuanza kwa vikundi vya kufanya usafi mitaani ambapo taka zote zinazozalishwa huzolewa na kuwekwa kwenye madampo ya muda ambayo yameongezeka na kufikia 40 kutoka 25 ya awali.


Mratibu wa mradi huo, Hawa Mshamu alisema wadau mbalimbali wana jukumu la kuunga mkono na kusaidia mkakati wa kuuweka mji huo katika hali ya usafi. Vifaa vilivyotolewa na mradi huo ni mafagi

Wednesday, February 8, 2012

Polisi yasaidiwa kompyuta kupambana na uhalifu mipakani Kigoma

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linalohusika na Uhamiaji (IOM), limetoa msaada wa kompyuta
sita kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma, ili kuimarisha utendaji kazi wake wa kupambana na vitendo vya uhalifu kwenye mipaka yake.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea vitendea kazi hivyo mwishoni mwa wiki, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Fraiser Kashai alisema vitasaidia katika kuimarisha hali ya ulinzi na usalama mkoani humo.


Kamanda Kashai alisema wakati huu wa zama za sayansi na teknolojia kuwepo kwa vitendea kazi hivyo kunawafanya wote wanaohusika na ulinzi na usalama kwa wananchi na mali zao kufanya kazi kama timu moja.


Alisema kompyuta hizo zitakazotumika kuwafundisha maofisa wa Polisi na Idara ya Uhamiaji zitaunganishwa pia na mtandao, zitakuwa msaada mkubwa katika kupata habari mbalimbali zikiwemo za wahamiaji haramu.


Akizungumzia kuhusu vifaa hivyo, Ofisa Miradi wa IOM, Marcelino Rumkishun alisema kompyuta hizo zina thamani ya Sh milioni 10 na ni sehemu ya mkakati wa shirika hilo katika kuisaidia mikoa minne ya Kanda ya Magharibi na Ziwa katika kupambana na vitendo vya uhamiaji haramu na wahalifu.

Kigoma wagumu kutoa taarifa za rushwa

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kigoma, imesema mwamko mdogo wa wananchi kujitokeza kutoa taarifa za vitendo mbalimbali vya rushwa katika jamii ni changamoto kubwa kwao inayokwamisha mkakati wa kupambana na vitendo
hivyo mkoani humo.

Mwanasheria wa Takukuru Mkoa wa Kigoma, Sweethbert Rwegasira alisema hayo wakati wa uzinduzi wa mradi wa utoaji wa elimu juu ya madhara ya rushwa kwa jamii unaoendeshwa na Shirika lisilo la kiserikali la Kioo katika kata nane za Wilaya ya Kigoma Vijijini kwa ufadhili wa Ubalozi wa Finland nchini.


Alisema vitendo vingi vya utoaji na upokeaji rushwa vinahusisha jamii kwa hiyo ili kupata uthibitisho wa vitendo hivyo, jamii inapaswa ishiriki kikamilifu kutoa taarifa kwa taasisi hiyo ili kuchukua hatua.


Alisema bila kupata msaada wa jamii katika kutoa taarifa kwao, Takukuru haiwezi kufanya lolote kwa sababu sehemu kubwa ya vitendo hivyo vinafanywa kwa makubaliano baina ya pande mbili, mtoaji na mpokeaji.


Alisema kuwepo kwa mradi huo kutasaidia taasisi yake katika kutekeleza mkakati wa utoaji elimu kwa jamii kuchukia vitendo vya rushwa, lakini pia wasaidie kutoa taarifa juu ya vitendo hivyo.


Kwa upande wake, Mratibu wa Shirika la Kioo, Edward Simon alisema Sh milioni 93 zinatarajia kutumika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ambao kwa kiwango kikubwa unalenga kuiwezesha jamii kujua madhara ya kutoa na kupokea rushwa katika utoaji huduma kwa jamii.