Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, September 12, 2012

AKAMATWA KWA KOSA LA KUSAFIRISHA BINADAMU

MKAZI wa Kijiji cha Kitema, Kata ya Nyakitonto, Yolam Venance (26), anashikiliwa na Idara ya Uhamiaji wilayani Kibondo mkoani Kigoma, kwa kosa la kufanya biashara haramu ya kusafirisha binadamu kutoka Burundi na kuwaingiza nchini kinyume na sheria.

Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Kibondo, Njunwa Mlaki, alisema walimkamta akiwasafirisha vijana saba wenye umri wa chini ya miaka 17 kutoka Burundi akiwapeleka wilayani Kasulu kwa ajili ya kwenda kufanya kazi ya kuchunga ng’ombe.

Aliwataja watoto hao waliokuwa wakisafirishwa kuwa ni Ngarukiye Fransis (16), Niyonkuru Erick (16), Nsimilimana Erick (11), Mubaimana Lamek (15), Sibomana Janemarie (15), Tivugwa Bimenyimana (15) na Imani Tharawis (11).

Baada ya vijana hao kukamatwa, Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Venance Mwamoto akiwa ameambatana na maofisa uhamiaji wamewasafirisha vijana hao hadi mpakani mwa Burundi na Tanzania na kuwakabidhi kwa Mkuu wa Wilaya ya Gisuru nchini Burundi, Ndikuliyo Egide, kwa ajili ya kuwarudisha nyumbani kwao.

Alisema idara yake ilipata taarifa kutoka kwa raia wema na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili wakati wowote ushahidi utakapokamilika.

Alisema Watanzania wanoishi mikoa ya mipakani hasa Kigoma na Kagera wanapenda kutumia nguvu kazi ya watu hasa kutoka Rwanda na Burundi kwa ajili ya kilimo na ufugaji.

Aliwataka Watanzania kufuata sheria na taratibu za uhamiaji za nchi na haki za binadamu wanapokuwa wanawaingiza watu nchini kutoka nchi mbalimbali.

No comments: