Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Wednesday, April 18, 2012

Hukumu ya akina Maranda Mei 17

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Mei 17, mwaka huu kutoa uamuzi katika kesi ya wizi wa Sh bilioni 2.2 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) fedha zilizokuwa zinatunzwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inayomkabili mfanyabiashara Rajab Maranda na binamu yake, Farijala Hussein.

Jaji Fatma Masengi ambaye ni mwenyekiti wa jopo linalosikiliza kesi hiyo, alisema hayo jana kesi hiyo ilipokuja kwa washitakiwa kujitetea na baada ya utetezi washitakiwa, wakili wao Majura Magafu kudai kuwa hana mashahidi wengine na pande zote mbili kudai kuwa hawana hoja za majumuisho.


Awali kabla washitakiwa kujitetea, Maranda aliomba mahakama hiyo kutupilia mbali mashitaka yote yanayomkabili kwa sababu hakuiba na pia hakughushi kama anavyodaiwa na Jamhuri na malipo yaliyofanyika kwenye kampuni yao ya Money Planner & Consultant Ltd kutoka kwenye akaunti ya EPA yalikuwa halali.


Alidai maelezo ya onyo anayodaiwa kukiri yasizingatiwe kwa sababu hakuwahi kuandika maelezo ya onyo anachokumbuka aliitwa na Tume ya Rais wakati wa uchunguzi wa tuhuma za EPA na alichohojiwa ilikuwa ni maelezo ya maisha yake kiujumla na aliitwa siku nyingine kusaini akaelezwa kuwa ni maelezo yale yale asaini tu haina haja ya kusoma.


Alidai Kampuni ya Money Planner & Consultant Ltd ilikuwa ikimilikiwa na Tobias Ng’ingo na Fundi Kitungo na walikuja kuomba msaada kwake wa Sh milioni 150 kwa ajili ya kufuatilia deni hilo, alidai baadaye aliwapatia fedha zile walikubaliana kuhamisha umiliki wa kampuni hiyo kuja kwa kwake na binamu yake.


Alidai mchakato wote wa kufuatilia deni hilo ikiwamo kuwasilisha hati ya kisheria ya kuhamisha deni BoT ulifanywa na watu hao na baada ya kukamilika, walirudi kwake ambapo walienda kufungua akaunti Benki ya BOA ili fedha ziingizwe.


Alidai zilipoingia alianza kulipa kulingana na maelezo aliyokuwa akipewa na kina Kitungo kwa sababu yeye alikuwa mtu wa kusaini hundi mara nyingi alisaini zikiwa hazijajazwa na kuziacha yeye alikuwa Kigoma.


Katika ushahidi wa Farijala, alidai alikutana na Kitungo akamueleza kuwa wamepata kazi ya kudai deni kutoka kampuni ya Ujerumani, aliwapeleka kwa Maranda na baada ya kukubaliana kuwamilikisha kampuni yao ambayo ndio iliyokuwa inatakiwa kulipwa deni hilo, walikubaliana malipo ni kugawana asilimia 40 ya kwao.


Alidai kwenda kubadilisha umiliki wa kampuni hiyo walifuatilia kina Fundi na baadaye waliwaeleza taratibu zimekamilika kampuni tayari iko katika majina yao.


Hata hivyo, kwa mujibu wa nyaraka alizooneshwa mahakamani na maswali na Wakili wa Serikali, Timoth Vitalis, ilionekana kuwa Maranda na Farijala waliingia ubia Desemba 5, 2005 na maombi ya kufungua akaunti BOA, yalianza Novemba 29, mwaka huo wakati akaunti hiyo iliingiziwa fedha na BoT, Desemba 7, mwaka huo ikionesha washitakiwa waliingia ubia wa Money Planner kabla ya kuanza mchakato wa kufungua akaunti ya deni.

No comments: