Karibu kwenye Blog ya Kijamii ya Kigoma yetu kwa habari na matangazo kwa bei nafuu sana. Tunakalibisha maoni, ushauri na habari zako ili tuijenge Tanzania kwa pamoja.

Tuesday, December 6, 2011

Polisi wanane mbaroni kwa kuua raia kinyama Kigoma

  • Wadaiwa kumtesa, kumpiga, kumdhalilisha hadharani
  • Wadaiwa kumpasua bandama kwa kitako cha bunduki
  • Mdogo wake naye yuko hoi mahabusu kwa kipigo 
     Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma,ACP Frasser Kashai.

    Askari hao wanadaiwa kumpiga kichwani na kwenye mbavu kwa kutumia kitako cha bunduki na kumwekea miti kwenye sehemu zake za haja kubwa.

    Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo katika Kijiji cha Rungwe Mpya, wilayani Kasulu Agosti 8, mwaka huu majira ya saa 8:00 mchana.

    “Askari wote wanane tunawashikilia na tunafanya uchunguzi juu yao waliohusika na tuhuma hizo za mauaji ya Festo Andrea, ikibainika watafukuzwa kazi na kupelekwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake,” alisisitiza Kamanda Kashai.

    Hata hivyo, alikataa kutaja majina ya askari hao kwa maelezo kuwa tuhuma hizo zinachunguzwa na kushughulikiwa na uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi na kwamba baada ya uchunguzi huo, yeye atapewa maagizo ili atoe taarifa kwa umma.

    BABA WA MAREHEMU ASIMULIA

    Akizungumza na NIPASHE nyumbani kwake katika Kijiji cha Rungwe Mpya, baba wa marehemu, Andrea Sama, alisema tukio hilo lilitokea Agosti 6, mwaka huu majira ya saa nne asubuhi katika kijiji hicho. 

    Sama alisema mwanaye huyo aliitwa na mgambo aitwaye Amosi Budida kwa maelezo kuwa anaitwa na afisa mtendaji wa kata kwa ajili ya kusajili bunduki yake na kuongeza kuwa walipofika ofisi ya kata walimfungia chumbani kwa madai kuwa polisi watakuja kumwambia kosa lake.

    Sama alifafanua kuwa baada ya muda, mdogo wa Festo , Sumbuko Andrea, alifika katika ofisi ya kata ili kujua kaka yake amekosa nini na ndipo na yeye aliingizwa katika chumba hicho na kuelezwa kuwa polisi watakuja kuwaeleza kosa lao.

    Mzee huyo alisema baada ya kuona watoto wake wote wawili wamefungiwa katika ofisi ya mtendaji wa kata, alikwenda katika ofisi hiyo ili kujua wamekosa nini mpaka wanafugiwa ndani.

    Aliongeza kuwa alipofika alimkuta afisa mtendaji wa kata na kuambiwa asubiri polisi watakapofika ili wamweleze kosa walilofanya wanawe.

    Alisema ilipofika saa 8:00 mchana, polisi wanane walifika katika ofisi ya mtendaji wa kata ambao ni Musa, Charles, Baraka, Shamsi na wengine wanne ambao hakuwatambua majina yao na kuhoji waliko watuhumiwa wao kisha kuwafungulia Festo na Sumbuko na kuwavua nguo zote kisha kuanza kuwapa kipigo kwa kutumia kitako cha bunduki, chupa za bia na kuwaingiza vijiti kwenye sehemu ya haja kubwa hadharani huku wananchi wakishuhudia pamoja na baba yao mzazi.

    Sama aliendelea kusimulia kuwa baada ya kuwapiga, waliwalaza ndani ya gari kifudi fudi kisha kuwawekea magunia manne ya mkaa juu ya migongo yao na kuondoka kuelekea Kasulu mjini.

    Alisema ilipofika saa mbili za usiku, alipata taarifa kuwa Festo amefariki na mwili wake uko katika Hospitali ya Wilaya ya Kasulu na Sumbuko yuko mahabusu kwa kosa la ujambazi wa kutumia silaha.

    Mzee huyo alisema: “Kitendo cha Polisi kuwaingiza vijiti watoto wangu wakiwa uchi wa nyama sehemu zao za haja kubwa na mimi nikishuhudia kwa macho yangu kinanisikitisha sana. Tangu nizaliwe sijawahi kuona polisi wanafanya unyama wa namna hii, siamini kama kweli polisi ni usalama wa raia na mali zao au ni kuua raia.

    “Naiomba serikali imwachie mtoto wangu Sumbuko ambaye anateseka gerezani bila kosa lolote. Kama serikali ilivyoniomba mimi nikapokea maiti ya mwanangu Festo na nikazika hivyo na mimi serikali inisaidie kunitolea mtoto wangu Sumbuko ili aje nyumbani aone kaburi la kaka yake kabla majani hayajaota,” alisema mzee huyo.

    KAULI YA DC

    Mkuu wa Wilaya ya Kibondo anayekaimu nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Danny Makanga, alisema: “Baada ya kutokea kwa mauaji ya Festo, niliunda kamati ya kuchunguza na mwenyekiti wake alikuwa Katibu Tawala Wilaya ya Kasulu, kamati hiyo ilinieleza kuwa kweli polisi wote wanane walihusika kumpiga Festo na kumsababishia kifo na kijana Sumbuko ambaye yuko gereza la Wilaya ya Kasulu ana makovu ya kipigo mwilini mwake hivyo namwachia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma kwa hatua zaidi za kisheria dhidi ya askari polisi waliohusika na mauaji hayo.”

    RIPOTI YA DAKTARI

    Daktari aliyeuchunguza mwili wa marehemu huyo, Dk. Said, alisema kuwa Festo alifariki kutokana na kipigo kilichosababisha kupasuka kwa bandama, michubuko usoni iliyosababisha kuvuja damu nyingi na jeraha kubwa sehemu ya kichwani.

    VIONGOZI WA KATA WAZUNGUMZA

    Diwani wa Kata ya Rungwe Mpya (CCM), Moris Zegeli, alithibitisha kutokea kwa mauaji ya Festo yaliyofanywa na askari polisi hao.

    Diwani Zegeli alisema: “Mimi ndiye niliyetoa gari langu kuchukua mwili wa marehemu Festo kutoka Hospitali ya Wilaya ya Kasulu kupeleka nyumbani kwao Kijiji cha Rungwe Mpya na kukuta wananchi zaidi ya 1,000 kwa kushirikiana na familia ya marehemu walikataa kuuzika mwili huo kwa saa nane kwa madai kuwa Polisi walimchukua Festo hapa kijijini akiwa mzima iweje arudi akiwa maiti.”

    Alisema kutokana na hali hiyo, viongozi mbalimbali wa serikali na wa vyama vya siasa waliwaomba wananchi pamoja na familia ya marehemu wakubali kuuzika na kuwaahidi kuwa Polisi waliohusika na mauaji hayo ya kikatili watachukuliwa hatua kali za kisheria.

    Alisema kuwa baada ya viongozi kusema hivyo, familia ya marehemu na wananchi walikubali kuuzika mwili wa Festo. Viongozi waliohudhuria mazishi hayo ni Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Kigoma; Mkuu wa Wilaya ya Kibondo; Diwani wa Kata ya Rungwe Mpya na na viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa katika kijiji hicho.

    Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Rungwe Mpya, Mosi Kilenge, alisema: “Mimi nimesikitishwa sana na kifo cha Festo kwani ni mchapa kazi sana hapa kijijini, hakuwa mlevi wala jambazi, naiomba serikali iwachukulie hatua kali askari polisi waliohusika na mauaji haya kwa sababu wanalidhalilisha Jeshi la Polisi na kuwafanya wananchi kuwachukia kwa vitendo vyao na kutoamini tena Jeshi hilo.”

    “Mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama katika kijiji hiki cha Rungwe Mpya, sijawahi kuwa na tatizo lolote na Festo hapa kijijini, naiomba serikali ichukuwe hatua askari polisi wote waliohusika na mauaji haya ili iwe fundisho kwa askari polisi wengine wenye tabia hizo za kikatili dhidi ya raia. Kwa kufanya hivyo, wananchi watalipenda Jeshi la Polisi,” aliongeza.

    Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advela Senso, alipoulizwa na NIPASHE kuhusu uchunguzi dhidi ya polisi wanaotuhumiwa kwa mauaji hayo, alisema alikuwa katika kikao na wakubwa wake.
     

No comments: