Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwahutubia wananchi wa Nguruka
wilayani Uvinza
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewaweka kitimoto wakurugenzi wa
Halmashauri ya Kasulu, Doroth Lwiza na Manispaa Kigoma/Ujiji, Boniface Nyambele
kuhusu fedha za barabara na elimu.
Amewataka watoe maelezo ya kutosha, kuhusu kushindwa kutumia
Sh bilioni tisa kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya barabara na uboreshaji wa
elimu.
Akizungumza katika siku ya mwisho ya ziara yake ya siku sita
mkoani Kigoma, Pinda awali alimtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji,
kueleza kuhusu kukwama kwa matumizi ya fedha hizo.
Alisema kitendo hicho kinachelewesha dhamira ya serikali ya
kuharakisha maendeleo kwa wananchi. Baada ya kutoa maelezo hayo, Waziri Mkuu
alimwita Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kasulu, Doroth Lwiza
akamtaka aeleze sababu ya kushindwa kutumia Sh milioni 897 kwa ajili ya
uendeshaji wa shule za msingi na sekondari.
Waziri Mkuu alisema taarifa alizonazo ni kwamba kiasi
kilichotumika hadi sasa ni Sh milioni 60, hivyo mipango mingi ya maendeleo
katika uboreshaji wa sekta ya elimu wilayani Kasulu, imekwama.
Akijibu kuhusu hali hiyo, Lwiza alisema mfumo wa matumizi ya
fedha unaotumia teknolojia ya intaneti, maarufu kama Epica, umechangia kukwama
kutumika na kutumwa fedha hizo katika maeneo husika.
Pinda hakuridhishwa na maelezo hayo na alimuagiza Waziri wa
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia kubaki mkoani Kigoma na
kushughulikia jambo hilo na baadaye ampe taarifa katika kipindi kifupi kijacho.
Alisema serikali haitawavumilia watendaji wachache kwa
sababu zao binafsi, kukwamisha mchakato wa serikali wa kuleta maendeleo ya
haraka kwa wananchi.